Waarabu wamhofia Samatta AFCON 2025
Muktasari:
- Tunisia ipo kundi moja na Taifa Stars huku timu nyingine zilizo kwenye kundi hilo C zikiwa ni Uganda na Nigeria.
Dar es Salaam. Benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tunisia, limemtaja Mbwana Samatta kama mchezaji wa kuchungwa zaidi katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazofanyika mwezi ujao nchini Morocco.
Katika Fainali hizo zilizopangwa kufanyika kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, Tunisia ipo kundi moja na Taifa Stars huku timu nyingine zilizo kwenye kundi hilo C zikiwa ni Uganda na Nigeria.
Kocha Mkuu wa Tunisia, Samy Trabelsi amesema kuwa Taifa Stars sio timu ya kubeza kwenye kundi hilo na wanapaswa kuikabili kwa umakini hasa kutokana na uwepo wa Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anachezea Le Havre inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.
"Tanzania inazidi kuimarika, huku klabu zikishiriki mara kwa mara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
"Wanaacha muonekano mzuri. Pia wana mchezaji bora, Ali Samatta, mshambuliaji bora ambaye amekuwa na maisha mazuri Ulaya," alisema Trabelsi ambaye amewahi pia kuichezea timu ya Taifa ya Tunisia miaka ya nyuma.
Mbali na Taifa Stars, Trabelsi amesema pia anategemea ushindani mkali kutoka kwa timu nyingine kwenye kundi hilo, Nigeria na Uganda.
"Nigeria inasalia kuwa nchi yenye nguvu barani, ikiwa na kundi kubwa la vipaji vinavyocheza katika vilabu vikubwa vya Ulaya.
"Uganda ni taifa linaloendelea kwa kasi. Walikuwa na kampeni thabiti ya kufuzu, hata kama mechi zao za kufuzu Kombe la Dunia hazikuwa za kipekee. Lakini kila mtu anakuja AFCON kwa lengo la kwenda mbali iwezekanavyo, na mara nyingi, timu zisizotarajiwa huzifunga timu kubwa," alisema Trabelsi.