Samatta kuandika rekodi mpya Ufaransa
Muktasari:
- Mbali na kucheza Ufaransa, Samatta aliweka rekodi ya kucheza Ligi Kuu England na kufunga bao akiwa Aston Villa 2020.
Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, kesho Agosti 16 ataandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza Ligi Kuu ya Ufaransa, baada ya kujiunga na klabu ya Le Havre AC inayoshiriki Ligi hiyo maarufu kama Ligue 1.
Agosti 5, mwaka huu klabu hiyo ilithibitisha kumsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja hatua ambayo ni mafanikio makubwa kwa mchezaji na taifa kwa ujumla.
Samatta, mwenye umri wa miaka 32, anajiunga na Le Havre baada ya kuachana na PAOK ya Ugiriki, akijiunga kama mchezaji huru ambapo mkataba wake ulimalizika Juni 2026.
Uhamisho huu unamfanya Samatta kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza Ligue 1, huku akiwa na historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza na kufunga kwenye Ligi Kuu ya England alipokuwa na Aston Villa mwaka 2020.
Katika safari yake ya soka Samatta aliwahi kucheza KRC Genk (Ubelgiji), Fenerbahçe (Uturuki), Royal Antwerp (Ubelgiji), na PAOK (Ugiriki). Akiwa Genk, alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi ya Ubelgiji. Ndani ya misimu minne akiwa Genk, alifunga mabao 76 na kutoa pasi 20 za mabao katika mechi 191 ikiwa ni sehemu ambvayo alifanikiwa zaidi.
Kabla ya kutimkia Ulaya Samatta alijizolea umaarufu akiwa na TP Mazembe ya DR Congo ambako alishinda mataji manne ya ligi na kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na yeye akaibuka mchezaji bora wa mwaka wa Afrika wa ligi za ndani.
Le Havre, moja ya vilabu vikongwe nchini Ufaransa, inatafuta kujiimarisha ili kuhakikisha inasalia kwenye ligi baada ya msimu uliopita kunusurika kushuka daraja ikimaliza katika nafasi ya 15, na kusajiliwa kwa Samatta kumechukuliwa kama usajili wa kimkakati ili kuisaidia klabu hiyo kufanya vizuri msimu ujao.
Kocha wa Le Havre, Didier Digard alisema, “Tumemfuatilia Samatta kwa muda mrefu. Ana kiwango bora na uzoefu wa kushindana katika Ligue 1.”
Samatta alisema kujiunga na Ligue 1 ni ndoto iliyotimia: “Uhamisho huu si kwa ajili yangu pekee, ni kwa kila mchezaji chipukizi wa Tanzania anayeamini kila kitu kinawezekana.”
Le Havre itashuka dimbani kutupa karata yake ya kwanza leo ambapo itakuwa na kibarua kigumu ugenini dhidi ya AS Monaco anayochezea nyota wa zamani wa Man United na Juventus, Paul Pogba na Ansu Fati ambaye ametokea Barcelona.