Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya nusu fainali CAF

Hesabu za kwenda fainali upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika zipo katika dakika 90 za kwanza wikiendi inayofuata ambapo mechi za hatua ya nusu fainali zitapigwa Aprili 10, 11 na 12 mwaka huu.

Mechi hizi za mkondo wa kwanza timu huzitumia vizuri kuchonga barabara, kisha marudiano kumalizia kazi na kama zikizingua mwanzo, huo ndio muda wa kurekebisha.

Jumla ya timu nane zinazoshiriki michuano hiyo ya CAF zilizotinga nusu fainali, zinafukuzia mkwanja mrefu ulioongezwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika kwa msimu huu wa 2025-2026, ambapo bingwa wa Ligi ya Mabingwa atajinyakulia Dola za Kimarekani milioni 6 (Sh15.6 bilioni za Tanzania) ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 kutoka zawadi za awali, huku bingwa wa Kombe la Shirikisho akiondoka na Dola za Marekani milioni 4 (Sh10.4 bilioni za Tanzania), ongezeko la asilimia 100 kutoka zawadi za awali.

Katika nusu fainali hizi, tunashuhudia mchanganyiko wa timu zenye historia ndefu, mabingwa wa zamani wanaorejea kwa kasi, na timu tishio zinazochipukia ambazo zimepindua meza ya matarajio.

Kubwa zaidi ni kwamba, Morocco ina wawakilishi watatu, wawili Ligi ya Mabingwa na mmoja Kombe la Shirikisho, huku Algeria inao wawili wote wakiwa Kombe la Shirikisho, Misri ina mmoja kama ilivyo kwa Tunisia na Afrika Kusini.


Ligi ya Mabingwa Afrika

Hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa inatupa picha kamili ya ubora wa soka la Kaskazini na Kusini mwa Afrika. Hapa kuna vita mbili kubwa; Mamelodi Sundowns dhidi ya Espérance de Tunis, na nusu fainali ya kusisimua ya timu mbili za Morocco, AS FAR dhidi ya RS Berkane.


Espérance vs Mamelodi

Huu ni mchezo unaokutanisha timu mbili ambazo zimekuwa na wakati mzuri katika miaka ya hivi karibuni. Espérance de Tunis, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakibeba kombe hilo mwaka 1994, 2011, 2018 na 2019, wameingia hatua hii kwa kishindo baada ya kuiondoa Al Ahly ya Misri, bingwa wa kihistoria, katika mchezo wa robo fainali.

Baada ya kushinda 1-0 nyumbani, Espérance walipambana na kushinda 3-2 ugenini, matokeo yaliyothibitisha kuwa wanalisaka kwa nguvu zote kombe la tano la michuano hiyo.

Upande wa pili, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini inaingia nusu fainali kwa mara ya nne mfululizo. Sundowns wametinga hatua hii baada ya kuiondoa Stade Malien kwa jumla ya mabao 3-2. Licha ya kupoteza 2-0 kule Bamako nchini Mali, ushindi wao wa kwanza wa 3-0 nyumbani Pretoria uliwatosha kusonga mbele. Kwa Sundowns, lengo ni moja tu, kunyanyua taji la pili la Ligi ya Mabingwa baada ya lile la mwaka 2016 walipowafunga Zamalek.

Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa timu hizi kukutana katika hatua ya mtoano, jambo linalofanya upinzani wao kuwa wa kipekee.

Mechi ya kwanza inachezwa Aprili 12 mwaka huu kwenye Dimba la Hammadi Agrebi Stadium jijini Tunis nchini Tunisia ambapo Esperance ni mwenyeji, huku Mustapha Ghorbal raia wa Algeria akipewa kazi ya kuwa mwamuzi wa kati.


AS FAR vs RS Berkane

Morocco imehakikishiwa mwakilishi katika fainali baada ya klabu zake mbili, AS FAR na RS Berkane, kupangiwa kukutana hatua ya nusu fainali, hivyo kwa vyovyote mmoja lazima acheze fainali kuliwakilisha taifa hilo.

AS FAR, klabu ya kwanza ya Morocco kushinda Ligi ya Mabingwa mwaka 1985, imerejea kwa kishindo kwa kuiondoa bingwa mtetezi, Pyramids FC ya Misri. Baada ya sare ya 1-1 kule Rabat, walionyesha nidhamu ya hali ya juu na ushindi wa 2-1 kule Cairo na kumvua Pyramids taji.

Wapinzani wao, RS Berkane, ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho, msimu huu wameamua kuonyesha makali yao katika Ligi ya Mabingwa.

Hii ni mara yao ya kwanza kufika nusu fainali ya michuano hii mikubwa. Berkane walifuzu baada ya ushindi wa dakika za majeruhi dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Timu hii inajivunia uzoefu wa michezo ya kimataifa ya hivi karibuni, ikiwa imeshinda mataji matatu ya Kombe la Shirikisho tangu 2020.

Kipute cha wapinzani hawa wa Morocco kitaamuliwa na mwamuzi, Dahane Beida raia wa Mauritania, wakati AS FAR ikiwa mwenyeji kwenye Dimba la Prince Moulay Abdellah jijini Rabat, Aprili 11, 2026.


Kombe la Shirikisho Afrika

Msimu huu michuano hii imejaa drama na matokeo yasiyotarajiwa. Nusu fainali itazikutanisha CR Belouizdad ya Algeria dhidi ya Zamalek kutoka Misri, wakati USM Alger ya Algeria ni dhidi ya Olympique Club de Safi kutoka Morocco.


CR Belouizdad vs Zamalek

Mchezo huu unawakutanisha Zamalek wa Misri wenye historia kubwa na CR Belouizdad ya Algeria inayotaka kurejesha heshima ya soka la nyumbani. Zamalek, ambao ni mabingwa mara mbili wa michuano hii (2019 na 2024), walifuzu baada ya mchuano mkali dhidi ya AS Otohô ya Congo, ambapo walishinda kwa jumla ya mabao 3-2. Safari yao msimu huu imejikita katika kurudisha hadhi yao barani.

CR Belouizdad kwa upande wao, wamefika nusu fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30. Walionyesha ukomavu kwa kuiondoa Al Masry ya Misri kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya 1-1 ugenini na 0-0 nyumbani.

Belouizdad wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya mwaka 2023 walipowafunga Zamalek mara mbili katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, jambo linalofanya mchezo huu kuwa wa kulipiza kisasi kwa upande wa Misri.

Dimba la Nelson Mandela pale Algiers nchini Algeria litapigwa pambano hili Aprili 10, 2026 na Abongile Tom kutoka Afrika Kusini akiwa mwamuzi wa kati.


USM Alger vs OC Safi

USM Alger ya Algeria, mabingwa wa michuano hii mwaka 2022-2023 na mabingwa wa CAF Super Cup 2023, wanaendelea na safari yao ya kutetea heshima hiyo. Walifuzu kwa shida dhidi ya AS Maniema Union ya DR Congo kwa sheria ya bao la ugenini baada ya sare ya 2-2 kwa jumla. Nidhamu yao ya ulinzi na uzoefu wa michezo mikubwa ndio silaha yao kuu.

Hata hivyo, wanakutana na timu ambayo ndiyo gumzo la michuano msimu huu, Olympique Club de Safi kutoka Morocco. OC Safi walishtua kwa kuiondoa klabu maarufu ya Wydad Casablanca katika robo fainali kwa jumla ya mabao 3-3, wakifuzu kwa faida ya bao la ugenini.

Safari yao imekuwa ya kusisimua, wakicheza soka la kushambulia kwa kushtukiza na kujilinda kwa pamoja, matokeo yaliyowaondoa vigogo wa Casablanca.

Aprili 11, 2026 mechi hii itachezwa pale Stade du 5 Juillet jijini Algiers nchini Algeris huku Mmisri, Amin Mohamed Omar akiwa mwamuzi wa kati.


Matarajio ya nusu fainali

Kitu kinachojitokeza wazi katika nusu fainali hizi ni utawala wa soka la Kaskazini mwa Afrika. Mataifa ya Morocco, Algeria, Tunisia, na Misri yametoa wawakilishi saba kati ya wanane katika hatua hizi mbili za nusu fainali. Mamelodi Sundowns pekee ndio wamebaki kupeperusha bendera ya Kusini mwa Afrika.

Katika Ligi ya Mabingwa, tunategemea kuona mbinu za kiwango cha juu. Sundowns watatafuta kutawala mpira kwa kutumia kiungo wao mahiri Teboho Mokoena na mlinda mlango Ronwen Williams ambaye amekuwa kiungo muhimu katika kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma.

Espérance kwa upande wao, chini ya kocha Maher Kanzari, wameimarika katika ulinzi na wanategemea kurejea kwa Mohamed Amine Tougai kuongeza nguvu.

Kwenye Kombe la Shirikisho, ushindani utakuwa katika umiliki wa kiungo. Zamalek watamtegemea mshambuliaji wao Oday Dabbagh mwenye mabao matatu msimu huu, huku USM Alger wakimtegemea mfungaji wao tegemeo Dramane Kamagaté.

OC Safi wanaweza kutumia mbinu ile ile iliyowaondoa Wydad, nidhamu ya hali ya juu na kasi ya mshambuliaji wao Soufiane El Moudane mwenye mabao manne nyuma ya kinara Abdennour Belhocini wa CR Belouizdad aliyefunga matano.