Vigogo Tanzania Bara kuhamishia vita Mapinduzi Cup 2026
Muktasari:
- Klabu ya mwisho kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ni Mlandege iliyofanya hivyo mwaka 2024 kwa kuifunga Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Dar es Salaam. Timu nane zitashiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 yatakayofanyika Visiwani Zanzibar mwanzoni mwa Januari.
Tanzania Bara itawakilishwa na klabu nne, Zanzibar itakuwa na klabu tatu na timu nyingine moja itatoka Uganda.
Klabu za Tanzania Bara zitakazoshiriki Kombe la Mapinduzi ni Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars.
Zanzibar katika mashindano hayo itawakilishwa na Mlandege, KVZ na Fufuni na klabu kutoka Uganda ni URA.
Waziri wa Waziri wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe amesema kuwa kutakuwa na ongezeko la zawadi katika mashindano hayo.
"Mshindi wetu wa kwanza atapata Shilingi za Kitanzania milioni 150 na Kombe la Ushindi na mshindi wetu wa pili atapata kiasi cha Shilingi za Kitanzania milioni 100. Mchezaji Bora wa mechi katika hatua ya makundi atapa Sh1 milioni, katika hatua ya robo fainali atapata Sh2 milioni na katika fainali atapata Sh3 milioni," amesema Pembe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kombe la Kombe la Mapinduzi, Makame Haji amewaomba mashabiki wa soka Zanzibar na Tanzania kiujumla kujitokeza kwa wingi viwanjani kutazama mechi za mashindano hayo.
"Nawaomba tusafiri pamoja katika jahazi hili ili tuweze kufikia malengo. Lengo kubwa ni kushajiisha hamasa ya michezo katika nchi yetu ya Tanzania na hapa Zanzibar," amesema Haji ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, sanaa, utamaduni na michezo.