Ushindi wa Arsenal waacha maswali EPL
Muktasari:
- Sare ilionekana kuwa matokeo ya mchezo hadi dakika ya 94, ambapo bahati iliwaangukia vinara hao wa Ligi Kuu England.
London, England. Arsenal imenusurika kupoteza pointi muhimu baada ya kuibuka na ushindi wa bahati dhidi ya Wolves ambayo ilijifunga mabao yote mawili, matokeo yaliyoacha maswali mengi kuliko majibu kwa kikosi cha Mikel Arteta.
Kwa namna mchezo ulivyokwenda, sare ilionekana kuwa matokeo ya mchezo hadi dakika ya 94, ambapo bahati iliwaangukia vinara hao wa Ligi Kuu England.
Usiku wa bahati kwa Arsenal
Hakuna aliyewapa Wolves nafasi yoyote. Pointi tatu zilionekana ndoto kwao, hata pointi moja ilikuwa miujiza. Hata hivyo, Arsenal iliondoka na pointi zote tatu baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1.
Bao la kwanza lilikuwa la bahati, kona ya Bukayo Saka ikigonga mwamba wa juu kabla ya kumgonga kipa Sam Johnstone na kuingia wavuni.
Wolves walirejesha matumaini dakika ya 90 kupitia bao la kichwa cha Tolu Arokodare, lakini furaha yao ilidumu kwa muda mfupi baada ya beki Yerson Mosquera kujifunga bao la ushindi kwa Arsenal.
Arteta amesema baada ya mchezo: “Tulizalisha nafasi nyingi za kufunga, lakini kulikuwa na dakika chache tulicheza kwa uzembe mkubwa wa ulinzi, kiwango ambacho hakiendani kabisa na mahitaji ya timu kama hii.”
Ni kweli kuwa kushinda hata ukiwa hujacheza vizuri ni sifa ya timu bingwa, lakini kuibuka na ushindi wa kubahatisha dhidi ya Wolves ni jambo linalotia wasiwasi kwa baadhi ya wachambuzi.
Arsenal ilionekana kukwama kabisa dhidi ya mbinu ya kujilinda kwa Wolves, wakishindwa kupenya ngome yao. Kwa mara ya kwanza msimu huu, walimaliza kipindi cha kwanza bila hata shuti moja lililolenga lango, hali iliyoongeza minong’ono ya kutoridhika kutoka kwa mashabiki.
Gyökeres aanza kutikisika
Ikiwa kulikuwa na mchezo ambao Viktor Gyökeres angeanza kuonyesha thamani yake, basi huu ulikuwa ndio. Wolves iliokuwa na pointi mbili tu kabla ya mechi walionekana kuwa wapinzani rahisi.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Sweden alishindwa tena kuudhibiti ulinzi Wolves. Alionekana kuchelewa kuipata mipira iliyovuka langoni na hakutumia ipasavyo nguvu zake kuwatoa mabeki kwenye nafasi.
Arteta amewataka watu wamwache apumue mshambuliaji huyo, ambaye ana mabao manne tu ya ligi katika mechi 14. Hata hivyo, kurejea kwake baada ya majeraha kumekuwa hakujaridhisha.
Kwa upande mwingine, Gabriel Jesus alionyesha kwa nini bado ana nafasi muhimu. Alipoingia dakika ya 81, aliongeza kasi ya ushambuliaji iliyosaidia kupatikana kwa bao la ushindi.
Jeraha jingine latikisa Arsenal
Orodha ya majeruhi Arsenal imezidi kuongezeka baada ya Ben White kuumia, akiwa wa saba kwenye safu ya ulinzi. White alishika paja la kushoto baada ya mbio za kasi kujaribu kumkimbiza Hwang Hee-Chan.
Arteta alikiri hali ilikuwa ya kulazimishwa: “Hatukuwa na chaguo. Tulilazimika hata kumchezesha Saliba kwa hatari. Hakuna mwingine.”