Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Urais TFF kaa la moto, kihunzi hiki hapa

Muktasari:

  • Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umepangwa kufanyika Agosti 16, 2025 ambapo nafasi saba zitawaniwa nazo ni moja ya Urais na sita za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.

Dar es Salaam. Hivi karibuni Kamati ya TFF ilitangaza ratiba ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo ambao ulianza Jumatatu, Juni 16, 2025 kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu na utakamilika Agosti 16, 2025 ambayo ndio siku ya uchaguzi wenyewe.

Nafasi saba zitawaniwa katika Uchaguzi huo Mkuu wa TFF mwaka huu ambazo moja ni ya urais na nyingine sita ni za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.

Kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi za TFF, mgombea wa nafasi yoyote kati ya hizo ambazo zimetangazwa anatakiwa kupata uungwaji mkono (endorsement) kutoka kwa wanachama wa TFF huku hilo likiwa ni takwa la kilazima.

'Endorsement' inapaswa kutolewa moja tu na kila mwanachama kwa nafasi husika na kwa mujibu wa katiba ya TFF, Wanachama wako 47 ambao ni Vyama vitano shiriki, Klabu 16 za Ligi Kuu na vyama vya soka vya mikoa.

Vyama vitano shiriki ni Chama cha Soka la Wanawake (TWFA), Chama cha Makocha wa Soka Tanzania (TAFCA), Chama cha wanasoka Tanzania (SPUTANZA), Chama cha Marefa wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na Chama cha Madaktari wa Tiba za Michezo (TASMA).

Kanuni ya 9:3 inatamka rasmi kuwa ni lazima kila mgombea ajaze fomu namba moja ambayo ndani yake inapaswa kuwepo na uungwaji mkono (endorsement) kutoka kwa wanachama wa TFF ambao wanaweza kuwa Vyama Shiriki au Timu za Ligi Kuu au Vyama 26 vya Soka vya Mikoa.


Urais kaa la moto

Kwa mdau wa soka ambaye ana ndoto za kuwania Urais wa TFF hapana shaka anakabiliwa na kibarua kigumu katika kusaka 'endorsement' kutokana na hitajio lisilo rahisi lan kanuni za uchaguzi kuhusu nafasi hiyo.

Ibara ya 30:4 ya Katiba ya TFF ikisomwa sambamba na Kanuni ya 9:4 inatamka wazi kuwa mgombea yeyote wa nafasi ya Rais wa TFF inapaswa kupata 'endorsement' zisizopungua tano toka miongoni wa Wanachama wake wote 47. Hili ni jambo la lazima.

Unafuu kidogo unaonekana kuwa kwa wagombea wa ujumbe wa kamati ya utendaji.

Ibara ya 30:8 ya Katiba ya TFF ikisomwa sambamba na Kanuni ya 9:5 inafafanua kwamba mgombea yeyote wa nafasi ya Ujumbe kamati ya Utendaji ya TFF anapaswa kupata angalau 'endorsement' moja toka miongoni wa Vyama vya Mikoa vilivyopo katika kanda anayogombea hili ni takwa la lazima kwa mgombea.

Ifahamike kwamba, mgombea mmoja wa nafasi ya Urais wa TFF, anaweza kupata 'endorsement' zaidi ya tano na maana yake ikitokea amepata 43, mgombea au wagombea wengine watajikuta wakilazimika kugawana endorsement nne tu hivyo kukosa sifa ya kikatiba kuwania nafasi hiyo kwenye uchaguzi huo.

Ikumbukwe katika Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika Kilimanjaro, Desemba 21, mwaka jana, wajumbe wa mkutano huo waliazimia kumpa Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia 'endorsement' zote na hilo liliibuka baada ya hoja iliyoanzishwa na klabu ya Simba kisha ikaungwa mkono na Yanga ya kutaka Karia aendelee kuongoza TFF.

“Dhumuni na dhamira rasmi ya kuwa na shirikisho kwamba ndio kilele cha uongozi wa soka katika nchi yetu. Umezungumzia mafanikio ya timu ya taifa ya vijana, timu ya taifa ya wakubwa, timu za taifa za wanawake, soka la ufukweni, hayo ndio mambo ambayo sisi wajumbe wako tunayatamani yawe yanatokea.

"Hoja yangu, katiba ya TFF Ibara ya 25(1) na Ibara ya 27(C) imetoa wigo mpana na mamlaka ya kimaamuzi ya mkutano mkuu huu. Maamuzi yanayofanywa na mkutano mkuu huu hayawezi kupingwa na chombo kingine chochote. Tanzania ni sifa yetu kutokuwa na ‘consistency’ (muendelezo). Tunaweza tukaanzisha jambo zuri lakini tukafika kati tukakwama.

"Wewe umefanya kazi nzuri sana tukupongeze. Kazi hiyo nzuri inastahili upewe tuzo. Chanda chema huvikwa pete na tuzo yenyewe uchaguzi wa Rais wa TFF mwakani unaoutaka wa nini? Mkutano ukuthibitishe leo. Hawa wajumbe wa kamati ya utendaji ndio tutakwenda kwenye uchaguzi lakini hili la rais kwanza tuwe tumemaliza, simamia hili jambo vizuri ili twende mbele. Ambaye atachukua fomu hiyo mwakani atakuja kutueleza jambo gani kubwa ambalo wewe umeshindwa kulifanya?,” alinukuliwa mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu.

Rais wa Yanga, Hersi Said aliunga mkono hoja hiyo na kusema kuwa hakuna sababu ya kufanya uchaguzi wa nafasi ya urais ili kutoa heshima kwa kile kilichofanywa na Karia.

“Mafanikio makubwa ambayo Rais pamoja na kamati ya utendaji ya TFF yamekuwa ni sababu kubwa ya maendeleo ya mpira wa miguu katika taifa letu. Sisi kama wadau wa soka katika taifa hili tunajivunia utendaji wako mheshimiwa Rais.

Kwa nafasi hii ndogo niliyopewa mheshimiwa Rais nikuhakikishie ya kwamba sisi wadau wa michezo tutaendelea kukuunga mkono wewe na kamati yako ya utendaji na nipongeze wazo zuri ambalo kaka yangu, Murtaza Mangungu amelitoa kwa asilimia mia moja. Kwa

Muktadha huo tutakuwa na uchaguzi wa idara nyingine kama za wajumbe wa kamati ya utendaji na sio eneo la rais,” alinukuliwa Hersi.


Akijibu maoni hayo, Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani alisema kwa dhana ya utawala bora, kufanyika kwa uchaguzi ni njia nzuri ingawa kinachoweza kufanywa na wanachama wa TFF ni wote kumdhamini Karia ili kusiwepo na mshindani mwingine katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.

“Kwanza ni hoja nzuri lakini tunaweza tukaiboresha ili tusivuruge katiba yetu. Takwa la uchaguzi ni takwa la kikatiba. Tunaweza tukahemewa tukatengeneza mazingira huko mikoani na wilayani huko kukawa na balaa zaidi.

“Kwa hiyo tunachoweza kufanya kwa vile rais wetu amefanya kazi kubwa na sisi ni mashuhuda wa kazi ambayo rais ameifanya. Na sisi ni masikini, hatuna mali ya kumuenzi rais wetu. Kumuenzi kwetu rais wetu ni kumuunga mkono sasa tunamuungaje mkono? Ndio hoja iliyopo mezani.

“Mtoa hoja alikuwa anazungumzia tumpitishe rais kwa azimio. Wanasheria wenzetu katika mambo ya utawala bora watasema haijakaa vizuri. Basi mimi nishauri, Katika kugombea urais wa TFF kuna takwa la kikatiba la kupata endorsement kutoka kwa wanachama wa TFF. Tukubaliane na kaazimio kidogo kwamba mkutano huu umeazimia kwamba wote tumpe endorsement rais atakapogombea,” alisema Nyamlani.

Kwa hali hiyo, mgombea yeyote wa nafasi ya Urais ya TFF mwaka huu, ana milima miwili ya kupanda ili atimize ndoto hiyo.

Kwanza ni kushawishi wanachama 47 wa TFF kutofanyia kazi kwa vitendo kile ambacho wamekubaliana katika mkutano mkuu uliopita wa TFF na akifanikiwa hapo, cha pili ni kuibuka kidedea katika sanduku la kura.

Tusubiri na kuona, muda utatoa majibu.