United yabanwa, Chelsea ikigawa dozi Ulaya

Muktasari:
- Tangu kuanza kwa msimu uliopita kipa wa United, André Onana ndiye anayeongoza kwa kufanya makosa mengi yaliyogharimu timu yake kuliko kipa mwingine wa EPL katika mashindano yote ambapo amefanya makosa nane.
Manchester United imelazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Europa League uliochezwa kwenye uwanja wa Groupama dhidi ya Lyon wakati Chelsea ikitamba kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Legia Warsaw katika mechi ya robo fainali ya Conference League.
Ilionekana kama Man United ingevuna ushindi wa ugenini baada ya Joshua Zirkzee kufunga bao dakika ya 88 yaliyoifanya itangulie kwa mabao mawili, lakini matumaini hayo yalizimwa na bao la dakika za nyongeza kutoka kwa Rayan Cherki.

Kocha Ruben Amorim amesema licha ya sare hiyo ya mabao 2-2, anaona dalili njema kutoka kwenye kikosi chake kuelekea katika mchezo wa marudiano wiki ijayo.
"Tulionesha juhudi na umoja. Tulistahili ushindi, lakini hii ni sehemu ya mpira. Tunaamini tunaweza kufanya vizuri nyumbani," amesema Amorim.
Lyon walitangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Thiago Almada katika dakika ya 25 kwa mpira wa adhabu, kabla ya beki, Leny Yoro kuisawazishia United kwa mpira wa kichwa akimalizia krosi ya Manuel Ugarte.

Kwa upande wa Chelsea, walitoa kipigo kizito kwa wapinzani wao baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 ugenini kwenye uwanja wa Polish Army dhidi ya Legia Warszawa.
Tryique George aliwafungulia njia The Blues kwa goli la kwanza katika dakika ya 49, kabla ya Madueke kufunga mabao mawili yaliyoiweka Chelsea katika nafasi nzuri kuelekea katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Stamford Bridge.

Maresca amepongeza nidhamu ya timu yake akisema kwamba bado kazi haijaisha.
"Tulicheza kwa akili na kasi. Ushindi ni mzuri lakini tunajua bado hatujamaliza kazi,” amesema Maresca.
Kwa sasa macho yote yameelekezwa kwenye mechi za marudiano wiki ijayo, huku Chelsea wakihitaji sare ili kusonga mbele, na United wakihitaji ushindi wowote ili kutinga katika hatua ya nusu fainali ya Europa League.