Raphinha aingia anga za Messi Barcelona

Muktasari:
- Raphinha amekuwa mchezaji wa kwanza kwenye mashindano ya UEFA kuhusika katika mabao zaidi ya 10 akifunga 12 na kutoa pasi saba za mwisho ndani ya msimu mmoja.
Barcelona. Nyota wa Barcelona, Raphinha jana ameweka rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo ilishuhudiwa Barcelona ikiifunga Borusia Dortmund mabao 4-0 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Olympic Luis, Hispania.
Mbrazili huyo alifunga bao la kuongoza katika dakika ya 25 kabla ya kutoa pasi ya bao la pili kwa Robert Lewandowski ambaye alifunga mabao mawili katika dakika ya 48 na dakika ya 66 akimalizia tena pasi ya Fermine Lopez.

Raphinha hakuishia hapo kwani katika dakika ya 77 alitoa pasi ya bao la nne kwa Lamine Yamal ambaye aliitimisha ushindi huo wa 4-0.
Baada ya kufunga bao na kutoa pasi mbili za mwisho, Raphinha ameingia kwenye rekodi ya kuhusika kwenye mabao 19 ndani ya msimu mmoja akiwa amefunga 12 na kutoa pasi saba za mwisho akiifikia rekodi iliyowekwa na Lionel Messi msimu wa 2011-2012.

Mchezaji mwingine ambaye aliweka rekodi kwenye mchezo wa jana ni Lewandowski, baada ya kuifunga Dortmund mabao mawili amekuwa mchezaji aliyeifunga timu hiyo ya Ujerumani mabao mengi akifikisha 29 kwenye michezo 28 ya mashindano yote.
Barcelona itarudiana na Dortmund, Aprili 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Signal Iduna Park, Ujerumani ambapo mshindi wa jumla atafuzu nusu fainali ya michuano hiyo.

Mchezo mwingine wa robo fainali uliochezwa jana ilishuhudiwa PSG ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa Parc des Princes jijini Paris, Ufaransa.
PSG ilitoka nyuma kwa bao moja baada Morgan Rogers kuitanguliza Aston Villa dakika ya 35 kabla ya Desire Doue kufunga bao la kusawazisha dakika ya 39 akimalizia pasi ya Nuno Mendes ambapo mapumziko matokeo yalikuwa 1-1.
Dakika ya 49, Khvicha Kvaratskhelia aliifungia PSG bao la pili kisha Nuno Mendes akahitimisha ushindi huo kwa bao alilofunga dakika za nyongeza baada ya kufika 90.

Msimu huu PSG imezifunga Manchester City, Liverpool na Aston Villa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiwa mara ya nne kuzifunga timu tatu za England kwenye mashindano hayo baada ya Bayern Munich kufanya hivyo msimu wa 2013-2014, Barcelona 2018-2019 na Real Madrid 2021-2022.
Ushindi ilioupata PSG unaifanya kwenda kifua mbele kwenye mchezo wa pili utakaochezwa Aprili 15, 2025 kwenye Uwanja wa Villa Park, England.