Rice aweka rekodi Arsenal ikiifunga Madrid

Muktasari:
- Arsenal ndiyo timu inayoongoza kufunga mabao mengi ya mipira iliokufa katika mashindano yote ambapo imefunga jumla ya mabao 21 msimu huu.
Mabao mawili aliyofunga Declan Rise na moja alilofunga Mikel Merino yalitosha kuipa ushindi wa mabao 3-0 Arsenal ambayo ilikuwa nyumbani kwenye uwanja wa Emirates dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Rice ambaye aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo, alifunga mabao yote mawili kwa mipira ya adhabu (Free kick) ambapo bao la kwanza alifunga dakika ya 58 huku la pili akifunga dakika ya 70.
Mabao mawili aliyofunga Rise yanamfanya awe mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili ya mipira iliokufa (Free kick) katika mchezo wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mchezo huo ilishuhudiwa Arsenal ikipata mabao matatu ndani ya dakika 17 baada ya Mikel Merino kufunga bao la tatu dakika ya 75.
Katika dakika za nyongeza Madrid ilipata pigo baada ya kiungo wake, Eduardo Camavinga kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyomfanya aonyeshwe kadi nyekundu hivyo atakosekana katika mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.
Tangu mwaka 2006 Luka Modric alipocheza kwenye uwanja wa Emirates akiwa na Dynamo Zagreb katika mchezo wa mtoano ilikuwa bado siku 34 beki wa Arsenal Myles Lewis Skelly azaliwe ambaye walikuwa wote uwanjani.
Myles Lewis Skelly amekuwa mchezaji wa pili kutoka England mwenye umri mdogo kucheza katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na miaka 18 na siku 194 baada ya Jude Bellingham kufanya hivyo mwaka 2021 akiwa na miaka 17 na siku 281.
Madrid inakibarua kigumu cha kupindua meza katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Aprili 18, 2025 kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo itahitaji ushindi wa mabao 4-0 ili ifuzu kwenye hatua ya nusu fainali.
Arsenal itaingia kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu ikiwa na mabao matatu huku ikiingia na rekodi ya kutofungwa kwenye uwanja huo ambapo mwaka 2006 iliiondoa Madrid baada ya kuifunga bao 1-0 katika hatua ya 16 bora.