Inter Milan yanukia nusu fainali Ulaya ikiichapa Bayern ugenini

Muktasari:
- Mshindi wa robo fainali baina ya Bayern Munich na Inter Milan, atakutana na mshindi baina ya Barcelona na Dortmund.
Inter Milan imejiweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Bayern Munich jana.
Mabao yaliyoihakikishia ushindi Inter Milan yamefungwa na Lautaro Martinez na Davide Frattes huku lile la kufutia machozi la Bayern Munich likipachikwa na Thomas Muller.
Kwa kupata ushindi huo, Inter Milan inahitaji ushindu au sare ya aina yoyote kwenye mechi ya marudiano wiki ijayo ili itinge nusu fainali.
Bayern Munich imepoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya nyumbani kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2021 ilipofanya hivyo dhidi ya PSG.
Kabla ya kupoteza jana, walikuwa wamecheza mechi 22 mfululizo bila kupoteza wakishinda 17 na kutoka sare 5.
Inter Milan imeshinda mechi tano mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu waliposhinda sita mfululizo katika msimu wa 2009/2010 ambao walitwaa ubingwa wakiwa chini ya Jose Mourinho.
Lautaro Martinez amekuwa mchezaji wa kwanza wa Inter Milan kufikisha mabao saba ktika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu Samuel Eto’o alipofanya hivyo msimj wa 2010/2011 alipopachika mabao nane.
Inter Milan imepata ushindi katika mechi tisa za ligi ya mabingwa Ulaya msimu ambayo ni idadi kubwa ya mechi walizoshinda katika mashindano ya Ulaya na wamerudia walichokifanya katika Kombe la UEFA msimu wa 1993/1994.
Bayern Munich imepoteza mechi nne za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ambayo ni idadi kubwa zaidi kwao kupoteza katika msimu mmoja tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2016/2017