Unai Emery akimbia kipigo kizito Arsenal
London, England. Unai Emery ametoweka kwenye benchi lake baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo ambao kikosi chake cha Aston Villa kilikumbana na kipigo kizito kutoka kwa Arsenal.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta hakutaka mchezo kwa kuamua kumsambaratisha Emery kwa kukichapa kikosi chake cha Aston Villa mabao 4-1 katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na hivyo kuweka pengo la pointi tano kileleni kabla ya mechi ya Manchester City.
Licha ya kukosa huduma ya kiungo wao wa Pauni 105 milioni, Declan Rice, Arsenal iliamsha dude kipindi cha pili na kufunga mara nne huku wafungaji wakiwa tofauti kabisa Gabriel Magalhaes, Martin Zubimendi, Leandro Trossard na Gabriel Jesus.
Straika Ollie Watkins aliifungia Aston Villa bao la kujifariji katika dakika za majeruhi huku kikosi hicho cha Emery kikitibuliwa rekodi yake ya kushinda mechi 11 mfululizo kwenye Ligi Kuu England.
Arteta, 43, alikwenda kumtafuta mpinzani wake huyo kwenye benchi lake la ufundi ili kupeana mikono baada ya mechi, lakini Emery hakuonekana, akiwa ameshatokomea vyumbani saa nyingi.
Arteta alionekana kwenye kamera za Sky Sports akimtafuta Emery bila ya mafanikio na mtangazaji wa Sky alisikika akisema: “Tunaona hapa marudio ya picha kwenye skrini yetu Mikel Arteta akijaribu kumtafuta Unai Emery bila ya mafanikio baada ya filimbi ya mwisho. Kinachoonekana kocha wa Aston Villa ameshaondoka kwenda vyumbani.”
Arteta aliulizwa kuhusu kutoweka kwa Emery baada ya mechi, kitu ambacho alijibu “hakuna shida” na kuongeza: “Wakati mwingine hivi vitu vinatokea, hivyo kwangu sio ishu.”