Ugumu wa kundi A CHAN uko hapa
Muktasari:
- Wenyeji Kenya ndiyo wanaongoza kundi wakiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi tatu.
Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani Afrika (CHAN), bado yanaendelea katika hatua ya makundi ambapo leo itachezwa michezo miwili ya kundi A inayopigwa nchini Kenya ambapo bado kuna nafasi ya timu zote kwenye kundi hilo kupenya hatua ya mtoano.
Mchezo wa mapema utapigwa saa 11: 00 jioni kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi Kenya utakaozikutanisha timu ya taifa ya Morocco dhidi ya Zambia.
Morocco ambao wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu wana kibarua kigumu cha kuhakikisha wanashinda mechi ya leo ili kufufua matumaini ya kucheza hatua ya mtoano.
Hadi sasa Simba wa milima ya Atlas wamecheza mechi mbili ambapo wameshinda moja dhidi Angola na kupoteza moja dhidi ya wenyeji Kenya.
Kwa upande wa Zambia ni kama upepo umewaendea vibaya kwani katika mechi mbili walizocheza zote wameambulia vichapo huku wakiburuza mkia kwenye kundi bila pointi.
Hata hivyo, Zambia bado wana nafasi ya kufanya vizuri na kufufua matumaini ya kwenda robo fainali iwapo watapata ushindi kwenye mchezo wa leo.
Lakini hilo linaweza lisiwe jambo jepesi, kwani ikitokea Zambia imepata ushindi leo basi itakuwa inaiombea dua mbaya Angola isipate ushindi dhidi ya DR Congo.
Angola inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne iwapo kama ikiifunga DR Congo basi itafikisha pointi saba ambazo hata Zambia ikishinda mechi mbili zilizobaki haiwezi kufikisha.
Kwa hesabu nyepesi tunaiona Zambia ikiwa na nafasi finyu sana ya kufuzu robo fainali kwani itatakiwa kushinda mechi zao mbili zilizobaki huku ikiziombea timu nyingine zipate sare mechi zao zote zilizobaki kitu ambacho ni kigumu kutokea.
Mechi nyingine itachezwa saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Safaricom Kasarani ambapo Angola itakabiliana na DR Congo.
Huu utakuwa ni mchezo mgumu kwani timu zote mbili bado zina nafasi ya kupenya katika hatua ya mtoano. Angola inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kuendelea kusalia kwenye nafasi hiyo.
Hata hivyo, nafasi ya Angola bado inaonekana kuwa ngumu kwani huu wa leo ni mchezo wao wa mwisho ambao hata wakipata ushindi watafikisha pointi saba ambazo zinaweza kufikiwa au hata kuvukwa na Morocco iwapo itashinda mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Zambia na DR Congo.
Mbali na Morocco timu nyingine ni DR Congo yenye pointi tatu ambayo pia inaweza kuipita Angola iwapo itafanikiwa kuifunga leo na kupata ushindi kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Morocco.
Hiyo basi, mshindi wa kwanza na wa pili kwenye kundi A atapatikana kwenye mechi za mwisho kutokana na ushindani uliopo kwenye kundi hilo ambalo hadi sasa timu zote zina nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano.
Katika hatua ya mtoano mshindi wa kwanza kwenye kundi B atakutana na mshindi wa pili kwenye kundi A kwenye robo fainali na mshindi wa pili kwenye kundi B atakutana na mshindi wa kwanza wa kundi A.
Pia mshindi wa pili kwenye kundi C atakutana na mshindi wa kwanza wa kundi D na mshindi wa kwanza wa kundi C atakutana na mshindi wa pili wa kundi D.