Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania inafeli hapa Olimpiki

Muktasari:

  • Riadha ni kati ya michezo yenye pesa nyingi, ambazo mchezaji anaweza kuvuna kutokana na kasi ya miguu yake inayoweza kubadili kabisa maisha yake, lakini pia kufungua fursa za kiuchumi.

Juzi Simbu alieleza namna ambavyo walishiriki mashindano ya Olimpiki huko Japan na kwamba alijitahidi kufanya kila namna ikiwa ni sehemu ya jukumu lake lakini haikusaidia, sasa endelea kufuatilia changamoto zingine wanazokumbana nazo....

Anasema: “Nafikiri kuna kitu hakikuwa sawa, yawezekana tulifanya sana mazoezi kupitiliza, sisi kwa kuwa tulikuwa tumeshakolea tuko kwenye moto, tukawa tunafanya tu.”


NYUMA YA PAZIA

Riadha ni kati ya michezo yenye pesa nyingi, ambazo mchezaji anaweza kuvuna kutokana na kasi ya miguu yake inayoweza kubadili kabisa maisha yake, lakini pia kufungua fursa za kiuchumi.

Kitendo cha Simbu kukomaa na kuingia 10 bora ya Olimpiki ni fursa kwake kupata mialiko ya kukimbia mbio kubwa za pesa ambazo kushiriki kwake tu ni pesa, achana na matokeo na kama atashinda ndio upepo wa maisha yake unaweza kubadilika kabisa na hata kuitangaza nchi kimataifa kupitia michezo.

Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni wakati akiipokea timu ya taifa ya Olimpiki, alisema nchi ya Argentina inatambulishwa duniani kupitia mambo makubwa yaliyofanywa na Lionel Messi na Diego Maradona kwenye soka, huku Kenya inao watu wengi akiwamo mwanariadha Eliud Kipchoge, hivyo akaitaka Tanzania iwe na utambulisho kwenye michezo.

Kwa kutoshiriki au kushindwa kuingia kwenye Top 10 ya Olimpiki, wanamichezo wengi wanapoteza fursa ya kualikwa kwenye mashindano mengine makubwa ya pesa nyingi.

Simbu hakurejea na medali, lakini ametunukiwa kwa mara ya pili cheti cha kimataifa na IOC kwa kuingia kwenye 10 bora ya Olimpiki, na siku si nyingi tutaanza kumsikia tena kwenye mbio kubwa kama ilivyokuwa ile ya London Marathon ya mwaka 2017.

“Olimpiki si riadha pekee, kuna ngumi, soka, kulenga shabaha na michezo mingine mingi, kule ndiko dunia yote ya wanamichezo inakutana, kutoshiriki kwetu kwa wingi kunatuchekewesha kimataifa,” anasema Simbu.


NINI KIFANYIKE?

Mwanariadha gwiji wa Tanzania, Selemani Nyambui anasema; “Hatuwezi kuendelea kwa kuwa na mbio lukuki za marathoni, huu ndio ukweli, hatuwezi kutengeneza timu ya taifa kutokana na mbio za marathoni zinazofanyika nchini.

“Hizo wanariadha wetu wanakimbia kutafuta pesa tu, na si mbio za kumuandaa kimataifa, ingewezekana kuwazuia wasishiriki hizo mbio ili watunze nguvu.

“Tukifanya hivyo, Serikali iamue wale tunaowategemea iwe inawalipa posho, ili sasa waachane na kukimbia hizo marathoni za nchini za kila wiki, kwani ni kweli watapata pesa ya zawadi, lakini zinawachosha mara kwa mara, bora ingekuwa ni moja kwa miezi mitatu au minne lakini sio kila siku,” anasema.

Anasema pia kuwe na mtu wa kuwahamasisha akitolea mfano wakati wao wakiwa kambini Arusha, rais wa wakati huo alimtuma aliyekuwa Waziri wa Michezo, Profesa Philemon Sarungi kwenda kuangalia timu inafanyaje mazoezi.

“Ukaribu wa viongozi wa ngazi za juu wa serikali kwa mchezaji kunaongeza hamasa kubwa sana, wakifanyiwa hivyo kabla na baada ya mashindano wanatambua thamani yao.

“Nakumbuka Rais Fidel Castro wa Cuba alikuwa anakunywa chai asubuhi na wachezaji wake baada ya mazoezi ambayo alikuwa akienda kuyashuhudia, hii iliwahamasisha sana, ndiyo sababu Cuba ilikuwa tishio kwenye ngumi duniani

“Hata sisi, wakati ule tulikuwa tunalelewa na taifa, ndio sababu tulifanya vizuri wakati ule,” anasema.

Anasema kilichoikwamisha Tanzania ni kutumia lugha ya “sasa tunajifunza”.

“Hii lugha imetutawala lakini bado tunakuwa hatujifunzi, tunapaswa kufanya vitu kwa vitendo, iwepo namna bora ya kupata wachezaji na kuwaendeleza.

“Tuna vipaji ambavyo vikipata kambi yenye utulivu, iwe na walimu wenye sifa, sio washika stop watch, bali makocha wenye sifa stahiki za kumpika mchezaji kutoka ziro hadi kuwa nyota, tutafanikiwa.”

Anasema kinachofanyika sasa ni kujifurahisha tu, akitolea mfano soka ambao Taifa Stars wanachuana kutafuta tiketi ya kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia.

“Kwenye soka sasa tunacheza ili tu kuifurahisha Fifa, lakini hatujawa tayari kufuzu Kombe la Dunia, labda tujipange kwa msimu mwingine lakini sio ujao, na hii ndio changamoto ninayoisema, tunashiriki tu, lakini hatuna malengo.

“Kufuzu Kombe la Dunia, labda tuanze kuandaa vijana tukiwa na lengo la miaka minane au 10 mbele, waachane na hawa wakongwe wa kusukumwa sukumwa tayari wamekomaa, binafsi sioni kama watatufikisha huko.”

Anasema tatizo jingine ni Tanzania kuwa sehemu ya kuwatengenezea masoko wachezaji wa mataifa mengine kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Tuangalie tu rekodi ya msimu miwili, wachezaji wetu waliotoka kwenda kucheza soka la kulipwa kulinganisha na wageni waliokuja kucheza ligi yetu, tunakuwa ni daraja la wageni kupita na kuonekana, lakini wa kwetu hawaendelei.

“Halafu tunaongeza idadi ya wachezaji wa kigeni hadi 12, tunapaswa kutoziangalia Simba na Yanga, tutengeneze wachezaji wetu, binafsi ningeambiwa wachezaji wangapi wa kigeni kwenye timu, ningependekeza watano na watatu ndiyo wapewe nafasi ya kuwa kwenye kikosi kinachocheza.

“Pia wachezaji wanane wa timu B wapandishwe na nusu wapate nafasi ya kucheza, kila timu ya Ligi Kuu iwe na timu ya vijana imara, kuwe na Ligi yao na tuanze kuwaandaa kwa ajili ya lengo fulani, tutafanikiwa na iwe hivyo hata kwenye michezo mingine,” anasema.


SERIKALI YAKIRI

Yusuph Singo ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini kwa nyakati tofauti aliiwakilisha Serikali kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2018 Scotland na Olimpiki ya 2021 Japan anasema alichokibaini Tanzania inakwama kwa kukosa maandalizi bora.

“Wenzetu wanaofanikiwa wanaandaa timu zao mapema, ndicho tunapaswa kufanya na sisi, tuwe na mpango wa maandalizi ya miaka minne.

“Olimpiki ya Paris (Ufaransa) 2024 maandalizi yaanze sasa, kuandaa timu mapema na kuanza maandalizi mapema, tuwe na makocha wenye sifa za kimataifa.

“Tujikite kwenye michezo ile sita ya kipaumbele kwa kuiangalia sana, ingawa hii haimaanishi tutaiacha mingine, hapana ila tutawekeza zaidi huko ambako hakuna shaka tukiipambania itatupa matokeo chanya kimataifa,” anasema.