Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamu, Chungu usajili wa Allan Okello Yanga

Muktasari:

  • Allan Okello mwenye umri wa miaka 25, ni zao la kituo cha kulelea vijana wenye vipaji vya soka cha klabu ya KCCA ya Uganda.

Muda wowote kuanzia sasa, Yanga itamtambulisha kiungo mshambuliaji, Allan Okello (25) kama mchezaji wake mpya akitokea Vipers ya Uganda.




Inaripotiwa kwamba imeilazimu Yanga kutumia kiasi cha Dola 300,000 kwa ajili ya kumnyakua kiungo huyo ambaye amekuwa akipendelea kutumia mguu wa kushoto.

Ni usajili ambao unaonekana una pande mbili za shilingi ambapo mmoja unaonyesha ni kwa nini Yanga imeshawishika kumnasa Okello na upande mwingine unaonyesha ni kama wa mtego kwa klabu hiyo.


MANUFAA YA OKELLO


1. Umri

Umri wa miaka 25 ambao Okello anao unaipa Yanga uwezekano wa kupata faida mbili kubwa ambazo klabu nyingi zimekuwa zikilenga pindi zinapofanya usajili wa wachezaji.


Kwanza ni kumtumia kwa muda mrefu kwa vile ana nishati ya kuweza kutumika kwa miaka 10 mbele lakini pili ni uwezekano wa kufanya biashara kwa kumuuza mchezaji huyo.

Yanga tayari ina historia ya kuonja fedha ya biashara ya mchezaji wa nafasi kama hiyo ambapo ilivuna zaidi ya Sh1 bilioni kwa kumuuza Stephane Aziz Ki kwenda Wydad AC ya Morocco mwaka jana.


Ubora na uzoefu

Okello ni mchezaji anayeweza kutumika kwa ufasaha katika nafasi tatu tofauti uwanjani na akatoa mchango mkubwa kwa timu ama kwa kufunga au kupiga pasi za mwisho.

Anaweza kucheza nafasi ya winga wa kushoto au kulia lakini pia akatumika katika nafasi anayoimudu vyema zaidi ya kiungo mshambuliaji.

Amekuwa na muendelezo wa kiwango bora kwa muda mrefu na takwimu zake zinathibitisha hilo.

Msimu huu tayari amehusika katika mabao matano kwenye mechi saba za Ligi Kuu ya Uganda alizoichezea Vipers, akifunga mabao matatu na kupiga pasi mbili za mwisho.

Msimu uliopita, alihusika na mabao 23 ya Vipers kwenye Ligi Kuu ya Uganda akifunga 19 na kupiga pasi tatu za mabao huku akiibuka Mfungaji Bora.


Ana uzoefu mkubwa wa kimataifa kupitia mechi alizoichezea Vipers na KCCA katika mashindano ya kimataifa na pia timu ya taifa ya Uganda aliyoitumikia katika michezo 36 na kuifungia mabao sita huku akipiga pasi 10 za mwisho.


Nidhamu

Allan Okello ni kijana mwenye nidhamu ya hali ya juu uwanjani na namba zinathibitisha hilo.

Hajawahi kuonyeshwa kadi yoyote akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Uganda na katika ngazi ya klabu, hajawahi kupata kadi nyekundu huku akionyeshwa kadi za njano tatu tu tangu alipoanza kucheza soka la ushindani hadi sasa.


MTEGO


1. Kutotumika kimataifa

Yanga italazimika kumsubiria Okello hadi msimu ujao ili imtumie katika mashindano ya kimataifa kwa vile msimu huu hawezi kucheza kwani tayari ameshaichezea Vipers kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga inashiriki pia.


2. Mazingira

Okello anakabiliwa na kibarua cha kukabiliana na mazingira ya ugenini ambayo yameonekana kumpa changamoto tofauti na anavyokuwa katika soka la Uganda.

Hii ni mara ya pili kwa nyota huyo kutoka nje ya Uganda ambapo mara ya kwanza aliitumikia Paradou ya Algeria kwa miaka miwili tu kisha kurejea Uganda baada ya kushindwa kumudu mazingira ya Algeria.


3. Dau la usajili

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho Yanga imekitumia kumsajili tena akiwa amebakiza miezi sita katika mkataba wake, kinaashiria shauku kubwa ambayo klabu hiyo imekuwa nayo ya kupata mafanikio kupitia Okello.

Hapana shaka dau la Dola 300,000 litamuweka katika presha kubwa ya kufanya vizuri kiungo huyo mshambuliaji ambayo kama akishindwa kukabiliana nayo, mambo yatakuwa magumu kwa upande wake.