Taifa Stars ndio basi tena, yaaga CHAN 2024
Muktasari:
- Taifa Stars ilimaliza ikiwa kinara wa kundi B la mashindano ya CHAN 2024 ikiwa na pointi 10 katika mechi nne.
Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeungana na Kenya kwa wenyeji wawili kutupwa nje ya Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo.
Bao la dakika ya 63 lililofungwa na mshambuliaji Oussama Lamlioui akipokea pasi ya kiungo Youssef Belammari, limetosha kusitisha matumaini ya Tanzania kubeba taji hilo ikiishia hatua ya robo fainali.
Tanzania itajilaumu yenyewe juu ya ubora wa safu yake ya ushambuliaji iliyoshindwa kutumia nafasi zilizotokana na makosa ya walinzi wa Morocco kwenye mchezo huo.
Licha ya Tanzania kutawala mchezo huo kwa vipindi vyote viwili, lakini mashambulizi yao yalikosa nguvu mbele ya ukuta wa Morocco.
Nafasi mbili kubwa ambazo Tanzania itazijutia ni Ile ya dakika za mwisho wa kipindi cha kwanza ambapo mshambuliaji Clement Mzize akiwa uso na kipa wa Morocco akashindwa kuchagua sehemu nzuri ya kufunga na kupiga mpira hafifu.
Kiungo Mudathir Yahya dakika ya 70 shuti lake lilitoka nje kidogo wakati Tanzania wakifika vizuri kwenye lango la Waarabu hao huku pia mshambuliaji Nassoro Saaduni aliyeingia kipindi cha pili akipoteza nafasi nzuri dakika ya 83.
Kutolewa kwa Tanzania linakuwa pigo la pili kwa wenyeji wa fainali hizo kutolewa ndani ya siku Moja ambapo mapema Kenya ikitangulia kutolewa iling'olewa kwa matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya kufungana bao 1-1.