Taifa Stars yafichua mkakati ya ushindi kwa Morocco
Muktasari:
- Taifa Stars ilimaliza hatua ya makundi ya Fainali za CHAN 2024 ikiwa kileleni mwa msimamo wa kundi B ikiwa na pointi 10.
Dar es Salaam. Benchi la ufundi na wachezaji wa Taifa Stars wameitangazia vita Morocco ambayo watacheza nayo leo kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024.
Wakizungumzia mchezo huo wa leo ambao utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa timu hiyo Hemed Suleiman ‘Morocco’ na beki Shomari Kapombe wamesema kuwa hawaihofii Morocco na wana imani watapata matokeo mazuri katika mechi hiyo.
“Tumekabiliana na timu nyingi kwenye haya mashindano na sasa tunatakiwa kuingia na mipango mingi tofauti ya mbinu.
“Kuna wakati mechi ni mbinu na mipango ya mbinu inaamua mechi. Itakuwa ni mechi ya wazi. Soka sio Bahati. Ni kuhusu utayari na sasa kocha anawafahamu wachezaji,” amesema Morocco.
Morocco amewatoa wasiwasi mashabiki na kuwaambia kwamba kikosi chake kipo tayari kwa mechi huku akiwaomba wajitokeze kwa wingi uwanjani leo.
“Katika mpira wa Miguu, mashabiki wanaweza kukupa vitu viwili, presha hasi na presha chanya. Kwetu uwepo wa mashabiki wetu unatupa hamasa na nishati ya kupata kinachohitajika. Kama tutaweza kuwapa kitu ili kuwafanya wawe na furaha, basi ni kufikia lengo lao,” amesema Morocco.
Beki Shomari Kapombe amesema wapo tayari kwa mechi hiyo ya leo.
“Kwa niaba ya wachezaji wenzangu tunasema tuajiandaa vizuri. Tupo tayari kwa asilimia 10. Morocco ni timu kubwa na hii ni fursa kwetu kuonyesha uwezo wetu. Tunaiheshimu hii timu lakini hatuiogopi,” amesema Kapombe.
Mshindi wa mchezo huo atakutana na timu itakayofanya vizuri katika mchezo baina ya Sudan na Algeria ambao utachezwa Zanzibar katika Uwanja wa New Amaan Complex.