Taifa Stars hesabu zinakubali kwa Ethiopia leo

Muktasari:
- Fainali za Afcon zinafanyika kila baada ya miaka miwili zikishirikisha timu za taifa 24
Muendelezo wa kufanya vizuri katika mechi za hivi karibuni unatoa matumaini kwa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kutamba dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco mwakani.
Taifa Stars inaingia katika mchezo huo ikiwa na takwimu bora kwenye mechi tatu mfululizo ilizocheza hivi karibuni ambapo imepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja.
Mei 19 iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sudan katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Saudi Arabia na Juni 2 ikatoka sare tasa na Indonesia katika mechi nyingine ya kirafiki na ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zambia, Juni 11.
Wakati Taifa Stars ikipata ushindi mara mbili na kutoka sare moja katika mechi tatu zilizopita, Ethiopia yenyewe kwenye mechi zake tatu zilizopita, imetoka sare mbili na kupata ushindi mara moja.
Matumaini makubwa ya Taifa Stars leo yapo kwa safu yake ya ulinzi ambayo katika siku za hivi karibuni imeonyesha ubora na muendelezo mzuri ambao umelifanya lango la timu hiyo kuwa salama mara kwa mara.
takwimu za mechi zilizochezwa hivi karibuni za timu hiyo za mashindano tofauti na kirafiki zinathibitisha uimara wa safu yake ya ulinzi.
Katika mechi 10 zilizopita, Taifa Stars imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu ikiwa ni wastani wa bao 0.4 kwa mchezo na mechi nyingine 10 kabla ya hapo, ilifungwa maba0 11 ikiwa ni wastani wa bao 1.1 kwa mchezo.
Taifa Stars inaingia katika mechi hiyo ikiwa haina historia nzuri dhidi ya Ethiopia ambapo katika mara 23 timu hizo zilipokutana, imeshinda sita, kutoka sare saba na kupoteza michezo 10.
Kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' alisema kuwa hawahofii kukutana na Ethiopia leo na watahakikisha wanapata ushindi.
"Tunajua tunacheza na Ethiopia timu ambayo kwa miaka minne, mitano hatujawahi kukutana nayo lakini ni nzuri inacheza kitimu lakini mimi naamini tuna malengo safari hii, tunataka kukutana na kila aliyepo mbele yetu hivyo tupo tayari kwa mchezo wa kesho (leo) alisema Morocco.
Beki wa Taifa Stars, Dickson Job alisema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi ya leo.
Kwa upande wetu sisi wachezaji tuko tayari kwa asilimia mia. Walimu tayari kazi yao wameshaimaliza katika viwanja vya mazoezi kwa hiyo kilichobakia ni kumuomba Mungu tuweze kuamka salama na tunawahakikishia Watanzania kwamba tutaenda kupambana kwa asilimia mia ili kuwapa furaha na tutaweza kupata matokeo mazuri," alisema Job.
Taifa Stars inatafuta tiketi ya kufuzu Afcon kwa mara ya nne baada ya kufanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023, wakati Ethiopia wanasaka tiketi ya kufuzu kwa mara ya sita baada ya kufanya hivyo mwaka 1957, 1962, 1982, 2013 na 2021, huku wakiwa na rekodi ya kubeba ubingwa mwaka 1962.
Ushindi katika mechi ya leo ambayo itaanza saa 1:00n usiku utaifanya Taifa Stars ikae kileleni mwa msimamo wa kundi H la kuwania kufuzu.
Timu mbili zitakazoongoza katika kundi H zitafuzu Afcon mwakani na mbali na Tanzania na Ethiopia, nyingine kwenye kundi hilo ni DR Congo na Guinea.
Matokeo ya michezo mitatu iliyopita baina ya Taifa Stars na Ethiopia
11/01/2013
Ethiopia 2 VS 1 Tanzania
28/11/2015
Ethiopia 1 VS 1 Tanzania
30/11/2015
Ethiopia 1 VS 1 Tanzania
Matokeo michezo mitatu ya Taifa Stars ya hivi karibuni.
11/06/2024
Zambia 0 VS 1 Tanzania
02/06/2024
Indonesia 0 VS 0 Tanzania
19/05/2024
Sudan 0 VS 1 Tanzania
Matokeo michezo mitatu ya Ethiopia ya hivi karibuni.
09/06/2024
Djibouti 1 VS 1 Ethiopia
06/06/2024
Guinea-Bissau 0 VS 0 Ethiopia
24/03/2024
Ethiopia 2 VS 1 Lesotho