Siku sita za moto kwa Taifa Stars

Kuna kipindi cha siku sita kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuchonga barabara ya kwenda Morocco kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 2025.
Siku hizo sita Taifa Stars itacheza mechi mbili za kufuzu Afcon 2025 dhidi ya Ethiopia na Guinea ambazo ni za Kundi H.
Taifa Stars mechi ya kwanza itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Septemba 4 mwaka huu dhidi ya Ethiopia, kisha siku sita mbele kwa maana ya Septemba 10 ni ugenini dhidi ya Guinea.
Ikiwa Kundi H, Taifa Stars kazi kubwa inayotakiwa kuifanya ni kuhakikisha hadi mwisho wa mechi hizo za kufuzu haitoki katika nafasi mbili za juu ili ipate nafasi ya kushiriki Afcon kwa mara ya nne kwani tayari imeshiriki mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 (Misri) na 2024 (Ivory Coast).
Tayari Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ametaja kikosi kilichoingia kambini kwa ajili ya mechi hizo mbili huku baadhi ya majina yakikosekana kama Mbwana Samatta na Simon Msuva.
Akizungumzia kikosi hicho kilichobeba matumaini ya Watanzania, kocha huyo aliyekabidhiwa mikoba ya Adel Amrouche ambaye aliweka pembeni tangu katika michuano ya Afcon iliyofanyika 2024, amesema anawaamini vijana wake wataifanya kazi vizuri.
“Najua kuwa Watanzania wangependa kuona wachezaji wengi wa Kitanzania ambao wanacheza soka la kulipwa nje wakiitwa lakini lazima wajue kuwa sisi kama walimu kuna mambo ambayo huwa tunazingatia na wachezaji wapo wengi hivyo orodha ingekuwa ndefu.
“Muda ni mchache sana kwa hiyo tumetazama wachezaji ambao wapo tayari moja kwa moja kuja kutumika, ni muhimu kuwa na wachezaji ambao wapo tayari sisi kama benchi la ufundi kazi yetu itakuwa kuingiza mbinu tu kwa ajili ya kutafuta matokeo katika michezo hiyo,” amesema kocha huyo na kuongeza.
“Kama Watanzania tunatakiwa kuwa kitu kimoja kipindi hiki katika kuisapoti timu yetu iweze kufanya vizuri na kuliletea taifa heshima, sisi sote tunataka kuona tunakwenda kushiriki tena Afcon hapo mwakani.”
Edwin Balua ambaye ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho, amesema kwake ni fahari kuona amejumuishwa kati ya nyota 23, hivyo atapambana kuisaidia nchi kufikia malengo.
“Ukipata nafasi ya kuiwakilisha nchi ni jambo kubwa na lazima ulichukulie kiukubwa na ukajitokea kwa asilimia mia moja, hilo ni jambo jema kwangu.
“Kama mwalimu amenichagua mimi kati ya wachezaji wengi basi kuna kitu amekiona kwangu na natakiwa kwenda kukionyesha, matarajio yangu kwenye timu ya taifa ni kuonyesha zaidi ya kile nilichofanya katika klabu yangu.
Watanzania watusapoti kwa sababu wao ni sisi na sisi ni wao, wanapotusapoti ni kitu kikubwa sana kinachotufanya kuendelea kupambana,” amesema Balua.
Kundi H lilivyo
Katika Kundi H, Tanzania imepangwa na timu za DR Congo, Guinea na Ethiopia. Ni kundi ambalo linazikutanisha nchi zenye wachezaji wanaofahamiana kwa namna moja ama nyingine, lakini pia ukiangalia katika viwango vya Fifa, DR Congo ndiyo ipo juu kuliko wapinzani wake ikishika nafasi ya 60.
Ethiopia ipo chini zaidi ikikamata nafasi ya 143, wakati Tanzania ni ya 113, kisha Guinea ipo 77. Hivyo ni viwango vya dunia kwa ujumla.
Ukiweka kando viwango hivyo vya Fifa, Guinea ina golikipa anayecheza Ligi Kuu Bara ambaye ni Moussa Camara aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Horoya AC, huku mshambuliaji wao kinara ni Serhou Guirassy anayeitumikia Borussia Dortmund inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani.
Kwa DR Congo, ni timu ambayo mara ya mwisho ilipangwa kundi moja na Tanzania katika michuano ya Afcon iliyofanyika Ivory Coast. Mbali na hilo, ni mataifa ambayo yamekuwa yakikutana mara kwa mara katika mechi za kimashindano siku za karibuni.
Pia hivi karibuni kumekuwa na lundo kubwa la wachezaji raia wa DR Congo wanaokuja kucheza Ligi Kuu Bara. Baadhi yao waliopo hivi sasa licha ya kwamba hawajaitwa kuitumikia timu ya taifa hilo ni Fabice Ngoma, Chadrack Boka, Maxi Nzengeli, Djuma Shaban na Heritier Makambo.
Hapo nyuma walikuwepo Fiston Mayele na Henock Inonga ambao wamekuwa wakiitumikia DR Congo mara kwa mara na walicheza Afcon iliyopita dhidi ya Tanzania.
Pia hata nyota wetu nao wapo DR Congo wanacheza, kwa sasa tunaye Abdallah Shaibu ‘Ninja’, pia Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Ramadhan Singano na George Mpole wamewaki kucheza huko.
Kidogo Ethiopia ni kama wageni mbele ya Tanzania kwani hakuna mchezaji hata mmoja kutoka taifa hilo anayecheza ligi yetu wala wa kwetu anayecheza kwao.
Ushiriki wa Taifa Stars Afcon
Katika ushiriki wake ndani ya michuano ya Afcon, Tanzania haijafanya vizuri huku mara ya kwanza mwaka 1980 ikimaliza mkiani mwa Kundi A baada ya kukusanya pointi moja ikiwa nyuma ya vinara Nigeria waliokuwa wenyeji na ndiyo mabingwa kwa mwaka huo, Misri na Ivory Coast walishika nafasi ya pili na tatu katika kundi lao.
Mwaka 2019, nchini Misri, Tanzania ilikwenda kushiriki Afcon kwa mara ya pili na kujikuta ikiondoka bila ya pointi baada ya kuwepo Kundi C na kumaliza mkiani dhidi ya timu za Algeria, Senegal na Kenya, kisha mwaka 2024 ikamaliza tena mkiani mwa Kundi F lakini safari hii iliambulia pointi mbili japo haikufanya vizuri.
Mtihani uliopo hivi sasa kama Tanzania itafuzu Afcon, ni kuona timu yetu inapanda nafasi na sio kuendelea kubaki mkiani kama ilivyokuwa huko nyuma, hiyo itaonyesha ukuaji wa kiwango cha timu yetu lakini pia nafasi haiwezi kupanda bila ya kufunga mabao. Kumekuwa na uhaba wa mabao kila Tanzania iliposhiriki Afcon.
Katika mara tatu ambazo Tanzania imeshiriki Afcon, imefunga mabao sita na kuruhusu 18 ikiwa ni kiwango cha chini zaidi kwa timu kukionyesha kwenye michuano. Mara ya kwanza ilifunga mabao matatu na kuruhusu sita, kisha ikafunga mawili na kuruhusu nane, huku 2024 ikifunga bao moja na kuruhusu manne.