Ratiba ya mtego Taifa Stars Afcon 2025

Muktasari:
- Katika droo ya upangaji makundi ya kuwania kufuzu Afcon 2025, Taifa Stars kwenye kundi lake hilo la H imepangwa pamoja na timu za DR Congo, Guinea na Ethiopia.
Dar es Salaam. Taifa Stars imepangwa kundi H katika mashindano ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Katika droo ya upangaji makundi ya kuwania kufuzu Afcon 2025, Taifa Stars kwenye kundi lake hilo la H imepangwa pamoja na timu za DR Congo, Guinea na Ethiopia.
Kwa mujibu wa Kanuni za mashindano hayo, timu mbili ambazo zitafanikiwa kuongoza msimamo wa kundi hilo pale hatua ya makundi itakapofikia tamati, zitafuzu kwa fainali za Afcon na mbili za mwisho zitatazama fainali hizo kupitia luninga.
Kalenda iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) inaonyesha kwamba mechi za hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Afcon 2025 zitaanza Septemba 2 na zitafikia tamati Novemba 19 mwaka huu, hivyo Taifa Stars itakuwa na siku 78 za kuhakikisha inapata tiketi ya Afcon mbele ya Guinea, Ethiopia na DR Congo.
Ratiba ya mtego
Taifa Stars itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kukabiliana na Ethiopia na baada ya hapo itakwenda ugenini kucheza na Guinea katika raundi ya pili ya mashindano hayo ya kufuzu.
Mechi ya tatu itakwenda ugenini kukabiliana na DR Congo na kisha ndani ya siku zisizozidi saba, timu hizo zitarudiana hapa Dar es Salaam.
Ikimalizana na DR Congo, itasafiri kwenda Ethiopia kuumana na timu ya taifa ya nchi hiyo katika mechi ya raundi ya tano na itamaliza mashindano hayo ya kuwania kufuzu kwa kupambana na Guinea hapa nyumbani.
Mechi za raundi ya kwanza na ya pili zitachezwa kuanzia Septemba 2 hadi 10, zikifuatiwa na zile za raundi ya tatu na nne ambazo zitafanyika kati ya Oktoba 7 hadi 15 na raundi mbili za kufunga dimba zitachezwa kati ya Novemba 11 na 19 mwaka huu.
Kimsingi kwa mujibu wa kalenda hiyo, raundi mbili zitakuwa zikichezwa ndani ya muda usiozidi siku nane (8) jambo ambalo litazifanya timu kuwa na muda mfupi wa maandalizi na mapumziko kutoka mechi moja hadi nyingine.
Kisasi cha Stars kwa wapinzani
Kutokuwa na historia nzuri dhidi ya DR Congo, Guinea na Ethiopia katika mechi zilizopita za mashindano tofauti ambayo Taifa Stars imewahi kucheza hapo nyuma, hapana shaka ni jambo lingine ambalo litaipa hamasa na morali zaidi Tanzania kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mechi za kundi hilo ili iweze angalau kulipa kisasi dhidi ya wapinzani hao mbali na hesabu za kutimiza lengo kuu ambalo ni kufuzu fainali zijazo za Afcon.
Taifa Stars imekuwa na unyonge dhidi ya DR Congo katika mechi za kimashindano ambapo katika mara saba ambazo zimewahi kukutana kwenye mashindano tofauti, imepata ushindi mara moja, imetoka sare mara tatu na kupoteza michezo mitatu.
Katika mechi za kimashindano, Guinea na Tanzania zimekutana mara moja tu ambayo ni katika fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) ambapo zilitoka sare ya mabao 2-2 lakini kiujumla zimekutana mara tatu, mbili zikiwa za kirafiki na zote Guinea ilipata ushindi.
Kihistoria Tanzania na Ethiopia zimekutana mara 18 katika mechi za mashindano tofauti ambapo Tanzania imeibuka na ushindi mara nne, zimetoka sare saba na Ethiopia imepata ushindi katika mechi saba.
Wapinzani wazoefu
Katika kundi hilo ni Tanzania tu ambayo imekuwa haina uzoefu mkubwa wa ushiriki kwenye fainali za Afcon na iwapo ikifanikiwa kumaliza katika nafasi mbili za juu, itakuwa imejihakikishia kucheza Afcon kwa mara ya nne baada ya kushiriki katika fainali za 1980, 2019 na 2023.
Mara zote ambazo Taifa Stars imeshiriki Afcon, haijawahi kuvuka zaidi ya hatua ya makundi na haijawahi kupata ushindi huku mafanikio yake makubwa yakiwa ni kukusanya pointi mbili.
DR Congo ndio timu yenye mafanikio zaidi kwenye Afcon mbele ya Guinea, Ethiopia na Tanzania kwa vile imetwaa ubingwa mara mbili, imeshika nafasi ya tatu mara mbili na ilimaliza katika nafasi ya nne mara mbili.
Katika kundi H, DR Congo ndio timu ambayo imeshiriki mara nyingi zaidi katika fainali za Afcon ambapo imefanya hivyo mara 20 na ikiwa itafanya hivyo safari hii itashiriki kwa mara ya 21.
Guinea imekuwa na uzoefu wa kutosha katika ushiriki wa fainali za Afcon na katika kundi H ipo nafasi ya pili kwa kushiriki mara nyingi nyuma ya DR Congo ikiwa imefanya hivyo mara 11.
Mafanikio makubwa ambayo Guinea imeyapata katika fainali za Afcon ni kumaliza katika nafasi ya pili ikifanya hivyo mwaka 1976 huku bingwa ikiwa ni timu ya taifa ya Morocco.
Ethiopia ni miongoni mwa timu zenye historia ya kuwahi kutwaa ubingwa wa fainali za Afcon ikifanya hivyo mara moja katika fainali za mwaka 1962 ilipoichapa Misri kwa mabao 4-2 katika mechi ya fainali.
Imewahi kumaliza katika nafasi ya pili mara moja ambayo ilikuwa ni mwaka 1957, mwaka 1959 ikishika nafasi ya tatu na katika fainali za mwaka 1963 na 1968 ilimaliza katika nafasi ya nne.
Matumaini makubwa
Nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Himid Mao alisema kuwa hawazihofii timu ambazao wamepangwa nazo kundi moja katika kuwania kufuzu fainali za Afcon 2025 na badala yake wana imani watakuwa miongoni mwa timu 24 zitakazoshiriki mashindano hayo huko Morocco.
"Tunaziheshimu DR Congo, Ethiopia na Guinea ambazo tumepangwa nazo kundi moja lakini hata na zenyewe zinatuheshimu sisi kwa vile tumekuwa tukifanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni. Mechi hazitokuwa rahisi kwa vile hakuna namna kila timu inaweza kufuu tofauti na kushinda mechi zake.
"Muda uliobakia ni mdogo lakini sisi kama wachezaji tutahakikisha tunajitoa kwa kadri ya uwezo wetu kuiwezesha timu yetu kupata ushindi ili tuweze kuingia Afcon kwa mara ya nne kwani kwa kushiriki mfululizo, tunazidi kupata uzoefu na ubora wa kimataifa," alisema Mao.
Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa shirikisho hilo litajipanga kuhakikisha Taifa Stars inafuzu kwenda Afcon huko Morocco.
"Malengo ya TFF na serikali ni kuhakikisha tunashiriki Afcon ya 2025 ili ituandae kwa ajili ya zile zitakazofanyika hapa nchini kwa kushirikiana na wenzetu Kenya na Uganda mwaka 2025. Muelekeo wa timu yetu kwa sasa unatupa matumaini ya kutimiza hilo na naamini kwa sapoti tunayoipata kutoka kwa serikali ambaye ni mdau namba moja na pia Watanzania kiujumla, tutaweza kufanikiwa," alisema Karia.