Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samatta, Msuva watemwa Stars, Job arudishwa

Muktasari:

  • Kwa upande wa makipa mkongwe Aishi Manula ambaye hajadaka kwenye mchezo wowote wa Simba msimu huu amepigwa chini, huku akiitwa Ally Salim kutoka Simba, Aboutwalib Mshery wa Yanga na kipa wa Pamba Yona Amos

Dar es Salaam. Kocha wa timu ya Taifa, 'Taifa Stars', Hemed Morocco amewatema wachezaji wakongwe kwenye kikosi hicho akiwemo nahodha Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Hii ni mara ya pili, Samatta anatemwa kwenye kikosi cha Stars baada ya kupigwa chini tena kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia, mchezo ambao Stars ilishinda bao 1-0.

Hata hivyo mchezo huo kiungo mshambuliaji ambaye alifanya vizuri kwenye michuano ya Afcon iliyopita Msuva alikuwepo lakini sasa naye ametemwa kwenye kikosi hicho ambacho kimejaa vijana wengi.

Hii ni mara ya kwanza Dickson Job anaitwa kwenye kikosi cha Stars tangu timu hiyo ilipotoka kwenye michuano ya Afcon mwanzoni mwa mwaka huu huku Morocco akisema kuwa wameshazungumza na wameelewana.

Kwa upande wa makipa mkongwe Aishi Manula ambaye hajadaka kwenye mchezo wowote wa Simba msimu huu amepigwa chini, huku akiitwa Ally Salim kutoka Simba, Aboutwalib Mshery wa Yanga na kipa wa Pamba Yona Amos ambaye ndiye pekee amekuwa akipata nafasi kwenye michezo mingi ya timu yake.

Amos alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba, mechi ambayo walicheza na Prisons na kumalizika kwa suluhu.

Hizi ndiyo zitakuwa mechi za kwanza za kufuzu kwa michuano hiyo ya Afcon 2025, ambapo Stars ipo kundi H dhidi ya DR Congo, Ethiopia pamoja na Guinea.

Stars itaanza kwa kuvaana na Ethiopia mchezo ambao kwenye ratiba ya CAF unaonekana utapigwa Septemba 2 kwenye Uwanja wa Mkapa na baadaye Septemba 10 itavaana na Guinea ugenini.

Wachezaji wengine walioitwa kwenye kikosi hicho ni Lusajo Mwaikenda, Nathaniel Chilambo, Mohammed Hussein, Pascal Msindo, Ibrahim Hamad Bacca, Bakari Mwamnyeto, Dikson Kibabage, Abdulmalick Zacharia, Adolf Mtasigwa.

Wengine ni Himid Mao, Novatus Dismas, Mudathir Yahaya, Hussein Semfuko, Edwin Balua, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Wazir Junior, Cyprian Kachwele, Clement Mzize na Abel Josiah.