Southampton yaongoza vita kumnasa Novatus

Muktasari:
- Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na timu hiyo msimu uliopita wa kiangazi akitokea Israel ambako alikuwa akiichezea Maccabi Tel Aviv na kuwashangaza wengi kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi.
Dar es Salaam. Licha ya chama lake, Zulte Waregem kushuka daraja huko Ubelgiji, kiungo wa Kimataifa wa Tanzania, Novatus Dismas ameziingiza vitani Southampton na Middlesbrough za England kupigania saini yake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na timu hiyo msimu uliopita wa kiangazi akitokea Israel ambako alikuwa akiichezea Maccabi Tel Aviv na kuwashangaza wengi kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi.
Akiwa na Zulte Waregem, Novatus ametumika kama beki wa kati, kushoto, winga na muda mwingine alicheza kama kiungo mkabaji nafasi ambayo Watanzania wengi wamezoea kumwona akicheza tangu akiwa kwa mkopo Biashara United ya Mara.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Southampton inayoshiriki Ligi Kuu England (EPL) ndio klabu inayoongoza vita hiyo huku wakifuatiwa kwa karibu na Middlesbrough ya Daraja la Kwanza 'EFL Championship' na wapo tayari kutoa Euro 550k (Sh 1.3bilioni).
Ikumbukwe ya kuwa Southampton ni miongoni mwa klabu za daraja la kati England ambazo zimekuwa zikilea na kuibua wachezaji wengi ambao wamekuwa wakifanya makubwa kwenye Ligi ya England mfano mzuri ni Sadio Mane ambaye alitamba akiwa na Liverpool kabla ya kwenda Bayern Munich, Virgil van Dijk.
Wengine ni Luke Shaw, Morgan Schneiderlin, Adam Lallana, Danny Ings, Dejan Lovren, Calum Chambers, Nathaniel Clyne, Jannik Vestergaard, Pierre-Emile Hojbjerg, Matt Targett, Graziano Pelle, Gareth Bale, Victor Wanyama, Oxlade-Chamberlain, Dusan Tadic, Jay Rodríguez.
Taarifa kutoka Ubelgiji, zinasema Zulte Waregem wanaweza kumwachia Novatus na winga wa Gambia Alieu Fadera ambaye anahusishwa na Manchester United katika dirisha hili la usajili ili kupata fedha ambazo zitawafanya kukiboresha kikosi chao kwa ajili ya kuanza maisha mapya ya Ligi Daraja la Kwanza Ubelgiji.
Novatus alicheza mechi 36 akiwa na Zulte Waregem msimu huu.
Hakufunga bao lolote lakini alitoa pasi mbili za mabao. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ni mchezaji wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na ameifungia mabao mawili.
WABONGO WAMKARIBISHA ENGLAND
Watanzania ambao wanaishi nchini England, John Makumba na Michael Stephano wamemkaribisha Novatus huku wakiombea dili hilo likamilike ili wamwone nyota huyo akicheza Ligi Kuu England kama ilivyokuwa kwa Mbwana Samatta.
"Tunatamani kuona wachezaji wengi wa Kitanzania kwenye ligi kubwa, hatukumfaidi kabisa Samatta kwa sababu alicheza kwa kipindi kifupi, kwa umri wa Novatus ni wazi kuwa tunaweza kumwona akicheza kwa muda mrefu zaidi," alisema Makumba.
Kwa upande wake, Stephano alisema,"Mimi kwanza naomba niweke wazi kuwa ni shabiki wa Arsenal na nimeumia sana msimu huu kukosa ubingwa wa Ligi Kuu ila nipo tayari kushabikia Southampton kama atasajiliwa huko (Novatus), lazima niwe mzalendo kwa mchezaji kutoka nyumbani."