Simbu aandika historia duniani akiipa Tanzania dhahabu
Muktasari:
- Kabla ya ushindi katika mashindano ya Dunia, Simba aling’ara katika mbio za Boston ambazo alishika nafasi ya pili.
Dar es Salaam. Felix Simbu ameitoa kimasomaso Tanzania baada ya kushinda medali ya dhahabu ya mashindano ya Riadha ya Dunia akimaliza katika nafasi ya kwanza upande wa mbio za Marathon Wanaume zilizofanyika usiku wa kuamkia leo huko Tokyo, Japan.
Simbu ameandika historia hiyo baada ya kumaliza mbio za kilomita 42 kwa saa 2:09.48 huku akipata upinzani mkali kutoka kwa Amanal Petros wa Ujerumani ambaye pia alikimbia muda sawa (2:09.48) na kushika nafasi ya pili, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Iliass Aouani wa Italia.
Mwanariadha huyo licha ya kumaliza muda mmoja na Petros ushindi wake umeamuliwa na teknolojia baada ya mguu wake kuwa wa kwanza kugusa ardhi baada ya kuvuka mstari wa mwisho.
Ushindi huo unamfanya Simbu kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama Mtanzania wa kwanza kushinda taji la Dunia katika riadha.
Kwa kupata ushindi huo, Simbu ana uhakika wa kupata kitita cha Dola 70,000 (Sh172 milioni) kutoka Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF).
Ukiondoa Simbu, Tanzania katika mbio hizo iliwakilishwa na Josephat Gisemo aliyeshika nafasi ya 53.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amempongeza Simbu na kumtaka aendelee kujituma zaidi.
“Hongera sana Alphonce Simbu kwa Medali ya Dhahabu ya ushindi wa Mbio Ndefu za
Mashindano ya Kimataifa ya Riadha ya Tokyo. Ndani ya saa 2:09:48 umeandika sehemu ya historia ya Taifa letu.
“Kama nilivyokusihi uliposhika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon mwezi Aprili mwaka huu, ushindi wako ni matokeo ya nidhamu yako ya hali ya juu na kujituma kwa bidii kwenye kazi.
“Umekuwa mfano bora kuhusu nguzo hizo mbili za kazi kwa wanariadha na wanamichezo wenzako, na hata kwa wasiyo wanamichezo,” amesema Rais Samia.