Mkenya ambwaga Assefa mbio za dunia Marathon, Simbu, Gisemo kukiwasha kesho
Muktasari:
- Mwanariadha anayefanikiwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia yanayoendelea Tokyo, Japan, anapata pia kitita cha Dola 70,000 (Sh172 milioni).
Mkenya Peres Jepchirchir ameibuka mshindi wa medali ya dhahabu kwa mbio za Marathoni Wanawake katika mashindano ya Dunia ya riadha yanayoendelea Tokyo, Japan akimbwaga Muethiopia Tigist Assefa.
Jepchirchir ambaye ametumia muda wa saa 2:24:43 kushinda mbio hizo ambazo zimeshirikisha wanariadha 73 kutoka mataifa tofauti duniani.
Nafasi ya pili imechukuliwa na Assefa aliyetumia muda wa saa 2:24:45 huku Julia Paternain wa Uruguay akimaliza katika nafasi ya tatu akikimbia kwa muda wa saa 2:27:23.
Ni ushindi ambao umeonekana kupokelewa vyema na Jepchirchir ambaye ameifanya Kenya kujibu mapigo kwa Ethiopia ambayo ilitawala mbio hizo awamu iliyopita upande wa wanawake.
Katika mashindano hayo upande wa wanawake awamu iliyopita, Ethiopia ilishinda medali ya dhahabu na fedha huku Kenya ikishindwa kupata hata moja.
Amane Shankule wa Ethiopia ndiye alitwaa medali ya dhahabu katika awamu iliyopita huku Muethiopia mwenzake Sutume Kebede akimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu ilichukuliwa na Fatima Gardadi wa Morocco.
Akizungumza mara baada ya kuibuka na ushindi, Jepchirchir amesema ni jambo ambalo hakulitarajia na limempa furaha iliyopitiliza.
“Kiukweli sikujua kama ningepata ushindi. Lakini nilipoona nipo Mita 100 kabla ya eneo la kumalizia, nilianza kuongeza kasi. Nilipata nishati ambayo ilijificha,” amesema Jepchirchir.
Baada ya wanawake kuonyeshana nani zaidi, hamu ya wengi ni kuona ni mwanariadha yupi atatamba upande wa Marathon Wanaume.
Katika Marathon wanaume, Tanzania itawakilishwa na wanariadha wawili ambao ni Alphonce Simbu na Josephat Gisemo.
Mbali na medali kwa washindi, mwanariadha ambaye anapata medali ya dhahabu katika mashindano hayo anavuta kitita cha Dola 70,000 (Sh172 milioni) huku mshindi wa pili akipata kiasi cha Dola 35,000 (Sh86 milioni) na anayeshika nafasi ya tatu anaondoka na kitita cha Dola 22,000 (Sh54 milioni).
Zawadi hizo za fedha haziishii kwa washindi watatu tu wa mwanzo bali pia hadi wale wanaomaliza katika nafasi ya nne hadi ya nane.
Wa nne anapata kiasi cha Dola 16,000 (Sh39 milioni), wa tano anaondoka na kitita cha Dola 12,000 (Sh30 milioni), kiasi cha Dola 8,000 (Sh20 milioni) kinaenda kwa atakayemaliza nafasi ya sita, wa saba atapata Dola 6,000 (Sh15 milioni) na wa nane atafutwa jasho kwa Dola 4,000 (Sh10 milioni).