Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yaichapa Mashujaa, uamuzi wageuka gumzo

Muktasari:

  • Licha ya kupata ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa KMC Complex, uamuzi wa mtanange baina ya Simba dhidi ya Mashujaa umegeuka gumzo kutokana na baadhi ya matukio yaliyojitokeza uwanjani hapo.

Dar es Salaam. Imeshuhudiwa kwa mara nyingine tena Simba ikiibuka na ushindi katika dakika za majeruhi baada ya kuifunga Mashujaa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwao uliochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Simba ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Steve Mukwala katika dakika za majeruhi.

Katika mchezo wa leo Mashujaa ndiyo ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa mshambuliaji, Jafary Kibaya katika dakika ya sita ambapo aliachia shuti kali liliomshinda kipa wa Simba, Moussa Camara.

Simba ilianza upya kutafuta bao la kusawazisha ikifanya mashambulizi mengi kwenye lango la Mashujaa bila kuzaa matunda yoyote.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika Mashujaa iliondoka ikiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa mchezo Simba.

Kipindi cha pili kilianza Simba ikifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji wake ambapo walitoka Edwin Balua, Awesu Awesu , Kelvin Kameta, Debora Fernandez na Valentin Nouma wakiwapisha Kibu Denis, Shomari Kapombe, Steven Mukwala na Joshua Mutale.

Simba kama ilivyomaliza kipindi cha kwanza ndivyo ilivyoanza kipindi cha pili kwa kupeleka mashambulizi mengi kwenye lango la Mashujaa mpaka ilipofika dakika ya 56 Simba iliandika bao la kusawazisha kupitia kwa Leonel Ateba ambaye alifunga kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Mashujaa kuushika mpira kwenye eneo la hatari.

Katika mchezo huo uliokuwa umejaa presha ilishuhudiwa golikipa wa Mashujaa, Patrick Muthary akionyeshwa kadi nyekundu yenye sintofahamu baada ya kumfuata refa wa mchezo pasipo kujua alimwambia kitu gani.

Abdulnasir Gamal ndiyo alichukua jukumu la kusimama langoni baada ya Mashujaa kumaliza kufanya mabadiliko.

Baada ya dakika 90 kumaliza ziliongenzwa dakika 15 za kufidia muda uliopotea ambapo katika dakika ya nne kati ya zilizoongezwa kipa wa Simba, Moussa Camara aliokoa mchomo mkali uliopigwa na mshambuliaji, Crispin Ngushi.

Dakika za jioni Simba ilipata bao la pili kupitia kwa Leonel Ateba ambaye alifunga kupitia mkwaju mwingine wa penati baada ya ya beki wa Mashujaa kumchezea rafu Shomari Kapombe ndani ya eneo la hatari.

Baada ya kupata ushindi huo Simba imesalia katika nafasi ya pili ikifikisha pointi 60 nyuma ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga inayoongoza kwa pointi 70.

Leonel Ateba baada ya kufunga mabao mawili amefikisha mabao 10 kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu akiwa nyuma ya Clement Mzize mwenye mabao 13, Jean Ahoua (12), Prince Dube (12) pamoja na Jonathan Souwah mwenye mabao 11.

Kabla ya mchezo kuanza ilishuhudiwa kocha wa Simba, Fadlu Davids na Steven Mukwala wakipata tuzo za kocha bora na mchezaji bora wa mwezi Machi.