Simba, Mashujaa FC hakuna mnyonge

Muktasari:
- Simba na Mashujaa zimekutana mara tano katika mashindano tofauti ambapo Simba imeibuka na ushindi mara tatu na Mashujaa FC imepata ushindi mara mbili.
Simba inaikaribisha Mashujaa FC kwenye Uwanja wa KMC Complex leo kuanzia saa 10:00 jioni katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu huku historia ya mechi za nyuma baina ya timu hizo ikifanya mechi hiyo kutotabirika kirahisi.
Hakuna utofauti mkubwa wa mechi za kushinda baina ya timu hizo katika mechi ambazo zimekutana hapo awali jambo ambalo linaashiria ushindani ambao zimekuwa zikionyeshana kila zinapokutana.
Timu hizo zimekutana mara tano katika mashindano tofauti ambapo Simba imeibuka na ushindi mara tatu huku Mashujaa FC ikipata ushindi mara mbili.
Wakati Simba ikiingia katika mchezo wa leo ikiwa na hesabu za kupata ushindi ili ifikishe pointi 60 ambazo zitaifanya iendelee kuipa presha Yanga iliyo kileleni mwa msimamo wa ligi kwenye mbio za ubingwa, Mashujaa FC inahitaji ushindi ili ijiweke katika mazingira mazuri ya kukwepa kushuka daraja.
Kocha msaidizi wa Mashujaa FC, Charles Fredie amesema kuwa wanajua ugumu wa kucheza na Simba hasa safu yao ya ushambuliaji lakini watahakikisha wanakabiliana nayo.
“Tunaamini pia safu yao ya ushambuliaji ni nzuri wana wachezaji wazuri ambao wanaweza kukuadhibu muda wowote kwa hiyo tumeiandaa timu vizuri kuweza kucheza nao kwa namna yoyote ile kuweza kuwakabili vizuri.
“Timu imeandaliwa vizuri kwa ajili ya kupata pointi tatu. Kiujumla changamoto itakuwa kubwa sana kwa sababu ni timu nzuri ambayo tunakutana nayo lakini sisi tumeandaa timu vizuri kukabiliana na Simba kwa hali yoyote ambayo watakuja nayo.
“Tumepata muda mwingi wa kuiangalia Simba mechi nyingi ilizocheza. Lakini hatuwezi kusema kwamba alivyocheza kwenye mashindano ya CAF ndio atacheza kwenye mashindano ya NBC Premier League,” amesema Fredie.
Kocha msaizidi wa Simba, Selemani Matola amesema kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wapo tayari kuicheza na kusaka pointi tatu.
“Tumefanya maandalizi yetu mazuri tukijua hatuna mchezo rahisi kwa sababu Mashujaa ni timu ambayo kiukweli imekuwa ikitupa wakati mgumu sana hata katika mechi yetu ya kwanza Kigoma walitupa wakati mgumu sana.
“Na ukiangalia wana mwalimu mzuri Salum Mayanga kwa hiyo nina imani ni mechi ambayo itakuwa na ushindani sana. Lakini kwetu sisi kwa sababu ni mechi za viporo tunazichukulia kama fainali hakuna mechi rahisi kwetu. Tumejiandaa pamoja na ubora wao na ugumu wanaotupa Mashujaa kwenye mechi tuhakikishe tunafanya vizuri.
“Tuna wachezaji ambao ni waelewa na nyakati hizi zote wameshawahi kuzipita kwamba mkitoka kwenye mechi ya kutumia nguvu kubwa kwa hiyo sisi walimu na wachezaji tumeliangalia na tumelifanyia kazi,” amesema Matola.
Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 57 ilizokusanya katika mechi 22 wakati huo Mashujaa FC ikiwa nafasi ya 10 na pointi zake 30