Yanga yakwama CAS, Kariakoo Derby kupangiwa tarehe

Muktasari:
- Mechi baina ya Yanga na Simba ya mzunguko wa pili Machi 8, haikuchezwa baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu.
Shauri lililofunguliwa na Yanga katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa michezo (CAS) kuomba mechi ya marudiano ya Ligi Kuu baina yao na Simba isipangiwe tarehe na pia ipewe pointi za mezani limegonga mwamba.
Mechi hiyo ilikuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu lakini ikaahirishwa baada ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku moja kabla ya mchezo.
CAS imeamua kutupilia mbali shauri hilo kwa vile Yanga haikufuata utaratibu wa kushughulikia malalamiko yake kwa kupeleka shauri hilo CAS kabla ya kuanza na vyombo vya ndani.
Katika majibu ya rufaa yake, CAS imeona haiwezi kuendelea na shauri hilo kwa vile Yanga haikufuata utaratibu kwa kufungua shauri kabla ya suala hilo kutolewa uamuzi na vyombo vya soka hapa nchini.
“Kwa hiyo, Naibu Rais anaona kuwa njia sahihi ya kukata rufaa ya Mrufani iko mbele ya Kamati ya Rufani ya TFF, na kwamba Mrufani alishindwa kutumia masuluhisho yote ya ndani ya kisheria kama inavyotakiwa na Ibara ya 37 ya Kanuni.
“Kwa hiyo, Naibu Rais anaona kwamba CAS haina mamlaka ya kutoa uamuzi kuhusu rufaa hiyo au kuhusu Ombi la Kutoweka lililowasilishwa na Mlalamikaji.
“Kwa kuzingatia hayo hapo juu, rufaa iliyowasilishwa na Young Africans Sports Club itachukuliwa kuwa imeondolewa na utaratibu wa CAS 2025/A/11298 Young Africans Sports Club dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania & Bodi ya Ligi Kuu Tanzania & Simba Sports Club utakatishwa na kufutwa kwenye orodha ya CAS,” imefafanua CAS.
Muda mfupi baada ya CAS kuamua hilo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kujiandaa kupanga tarehe ya mechi hiyo.
“МАНАКАМА ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imetupa rufani ya klabu ya Yanga yenye kumbukumbu namba CAS 2025/A/11298 ambayo klabu hiyo iliifungua dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC).
“Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ambapo pamoja na mengine, klabu ya Yanga iliomba mechi tajwa hapo juu isipangiwe tarehe mpaka litakapotolewa uamuzi, ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (PLB), na klabu ya Simba.
“Kutokana na uamuzi huo wa CAS, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaendelea na maandalizi yake ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2024/2025 na kufanya maboresho ya ratiba ya Ligi (ukiwemo mchezo namba 184 - Young Africans vs Simba SC) kisha kutangaza ratiba mpya mapema iwezekanavyo,” imefafanua taarifa ya TPLB