Simba kuzoa mabilioni fainali Shirikisho Afrika

Muktasari:
- Mara ya mwisho kwa Simba kuingia katika hatua ya fainali ya mashindano ya Klabu Afrika ilikuwa ni 1993 ambapo ilifanya hivyo katika Kombe la CAF na ilifungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan katika mechi mbili baina yao.
Dar es Salaam. Simba imeandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga mara nyingi fainali za mashindano ya klabu Afrika baada ya jana, Aprili 28 kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare ugenini dhidi ya Stellenbosch huko Afrika Kusini na kwa kutinga hatua hiyo ina uhakika wa kupata fedha za maana kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kama itafanikiwa kuchukua ubingwa wa mashindano hayo, Simba itazoa kiasi cha Dola 2 milioni (Sh5.4 bilioni) ambapo asilimia 10 ya fedha hizo kwa mujibu wa utaratibu itaenda kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Ikimaliza katika nafasi ya pili, Simba itazoa kiasi cha Dola 1 milioni ambacho kwa fedha ya Tanzania ni sawa na Shilingi 2.7 bilioni na utaratibu ni uleule wa TFF kupata aslimia 10.
Simba imetinga hatua ya fainali kwa kubebwa na ushindi wa bao 1-0 ambao imeupata nyumbani katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumapili iliyopita, Aprili 20 mwaka huu.
Hiyo ni mara ya pili kwa Simba kuitupa nje timu kutoka Afrika Kusini kwenye mashindano yab klabu Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2003 ilipoitoa Santos ya Afrika Kusini katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa kutinga fainali, Simba inaandika rekodi ya kuwa timu ya Tanzania iliyofika hatua hiyo mara nyingi zaidi katika mashindano ya klabu Afrika.
Hii ni mara ya pili kwa Simba kuingia hatua ya fainali ya mashindano yaliyochini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 1993 ilipoingia katika hatua ya fainali Kombe la CAF na hivyo ndio timu ya Tanzania iliyoingia hatua hiyo mara nyingi kwenye mashindano ya klabu Afrika.
Kwa Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ni timu ya pili kuingia hatua hiyo ya fainali, ya kwanza ikiwa ni Yanga iliyofanya hivyo katika msimu wa 2022/2023.