Simba yatinga kitemi fainali Shirikisho Afrika

Muktasari:
- Bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika anapata kitita cha Dola 2 milioni na mshindi wa pili anapata kiasi cha Dola 1 milioni.
Sare ya bila kufungana dhidi ya Stellenbosch ugenini kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban Afrika Kusini leo Aprili 27, 2025 imeivusha Simba kwenda hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikibebwa na ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mechi ya kwanza nyumbani Jumapili iliyopita.
Stellenbosch ambao katika mechi nyingi za mashindano hayo wamekuwa wakicheza kwa kutegemea mashambulizi ya kushtukiza, katika mchezo wa leo walionekana kuingia tofauti ambapo walimiliki mpira na kushambulia kwa muda mrefu lakini safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa imara kuondosha hatari ambazo ilielekezewa.
Katika mchezo huo, kulikuwa na matukio mawili makubwa ambayo yalimlazimisha refa Mohamed Maarouf Eid Mansour kutoka Misri kwenda kutazama marejeo kupitia teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) na kulazimika kubadilisha uamuzi wa awali.

Tukio la kwanza lilikuwa ni dakika ya 11 ambapo refa huyo aliizawadia Simba mkwaju wa penalti baada ya awali kudhani Kibu Denis aliangushwa katika eneo la hatari lakini baada ya kulitazama upya tukio hilo, alibatilisha uamuzi wake.
La pili lilikuwa katika dakika ya 78 ambapo Genino Palace aliifungia bao Stellenbosch lakini mwamuzi Mansour alilibatilisha baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na tukio la kuotea wakati bao hilo linatengenezwa.
Licha ya Stellenbosch kuongeza kasi ya mashambulizi, Simba ilionyesha uimara katika kujilinda na ikawanyima wapinzani wao fursa ya kufunga bao hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.

Ushindi huo unaifanya Simba itinge kwa mara ya pili hatua ya fainali ya mashindano yaliyochini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 1993 ilipoingia katika hatua ya fainali Kombe la CAF.
Kwa Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ni timu ya pili kuingia hatua hiyo ya fainali, ya kwanza ikiwa ni Yanga iliyofanya hivyo katika msimu wa 2022/2023.
Katika hatua ya fainali, Simba itaanzia ugenini na itamalizia nyumbani.
Kwenye mechi ya leo, Simba ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu na Mohamed Hussein ambao nafasi zao zilichukuliwa na Debora Fernandes, Valentine Nouma, Leonel Ateba na Che Fondoh Malone.
Stellenbosch iliwatoa GeninoChumani Butsaka, Khomotjo Lekoloane, Enyinnaya Godswill na Sile Nduli ambao nafasi zao zilichukuliwa na Lesiba Nku, Cheswyn Philander, Sanele Barns na Genino Palace.