Diadora kutengeneza jezi Simba

Muktasari:
- Mkataba baina ya Simba na Jayrutty Investment ni wa miaka mitano wenye thamani ya Sh38 bilioni.
Dar es Salaam. Kampuni ya kimataifa ya uzalishaji wa vifaa vya michezo ya Diadora ya Italia ndio itabuni na kuzalisha jezi na bidhaa nyingine zenye nembo ya Simba kwa miaka mitano baada ya kuingia mkataba na kampuni ya Jayrutty Investment.
Jayrutty Investment ndio kampuni yenye haki za matumizi ya nembo ya Simba kuzalisha jezi na bidhaa nyingine zenye nembo ya klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Sh38 bilioni.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kuwa kitendo cha jezi na bidhaa zao kuzalishwa na Diadora ni jambo la heshima kubwa kwao.
“Diadora ni ‘brand’ (chapa) kubwa duniani imewahi kuvaliwa na timu kama timu ya taifa ya Italia wakati ule inabeba Kombe la Dunia, AS Roma ya Italy na timu nyingine kubwa duniani.
"Simba Sports Club inazidi kukua na kuwa brand kubwa ya kimataifa hivyo ni lazima tushirikiane na brand kubwa kuonesha ukubwa wetu,” amesema Mangungu.
Naibu waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amesema amefurahi kuona mkataba wa Simba na Jayrutty unatekelezwa vyema.
"Nimekuja hapa kushuhudia ule utekelezaji wa yale yaliyosemwa wakati wa utiaji saini ya Uzabuni na
Kampuni ya JAYRUTTY Investment, mmeonesha ya dhati kutekeleza mliyokubaliana.
"Mwenyewe nilikuwa na shauku ya kuijua hiyo brand kubwa ambayo mlisema itaivalisha Simba
Sports Club ila leo nimekubali kweli ni brand kubwa, Diadora ni brand kubwa Duniani,” amesema Mwinjuma.