Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yaambulia nafasi ya tatu Ngao ya Jamii

Muktasari:

  • Kocha huyo alipangua kikosi kilichopoteza mbele ya Yanga kwa kuwapumzisha nyota wanne na timu kucheza soka safi dakika 45 kipindi cha kwanza

Bao pekee lililowekwa kimiani dakika ya 10 tu ya mchezo na kiungo mshambuliaji, Saleh Karabaka imeiwezesha Simba kumaliza katika nafasi ya tatu katika michuano ya Ngao ya Jamii mbele ya Coastal Union, huku kocha Fadlu Davids akilalamika timu yake kushindwa kutumia nafasi za kufunga.

Kocha huyo alipangua kikosi kilichopoteza mbele ya Yanga kwa kuwapumzisha nyota wanne na timu kucheza soka safi dakika 45 kipindi cha kwanza.

Simba iliyopoteza mechi na taji la Ngao ya Jamii ilipovaana na Yanga katikati ya wiki iliyopita, jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilitembeza soka tamu lililowapa burudani mashabiki wa timu hiyo, wakati ikishinda bao 1-0 na kumaliza kama mshindi wa tatu wa michuano hiyo lakini ikipata upinzani toka kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa wengi uwanjani wakisubiri mchezo wa fainali waliokuwa wanaiunga mkono Coastal Union.

Karabaka alifunga bao hilo akimalizia mpira wa krosi ya Steven Mukwala iliyoguswa na Joshua Mutale na mfungaji huyo kukwamisha kwa shuti la karibu lililoshinda nguvu kipa Chuma Ramadhani aliyeanzishwa katika mchezo huo kuchukua nafasi ya Athuman Msekeni aliyepigwa mabao 5-2 na Azam visiwani Unguja.

Ngoma aanza

Katika pambano hilo, dakika 10 za mwisho zilikuwa za presha kwa wachezaji wa timu hizo, huku buti likitembezwa kwa timu zote na kuifanya Simba kumaliza ikiwa pungufu baada ya kiungo Fabrice Ngoma kuonyesha kadi ya pili ya njano iliyosindikizwa na nyekundu kutoka kwa mwamuzi Ramadhan Kayoko.

Ngoma alipewa kadi nyekundu, baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Coastal, Mbaraka Yusuph wakati anaenda kumsalimia kipa Moussa Camara, huko njano zikitoka kwa wachezaji wengine.

Hii ina maana kuwa Ngoma ataukosa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United.

Licha ya Simba kucheza pungufu dakika 10 za mwisho ukichanganya na nne za nyongeza, ilifanikiwa kulinda ushindani wa bao la kwanza na kutangazwa mshindi wa tatu wa michuano hiyo.

Simba iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0, kutoka kwa wapinzani wao Yanga katika mchezo wa nusu fainali iliyopigwa Agosti 8 huku Coastal wakipigwa 5-2 na Azam.


Mchezo ulivyokuwa

Simba ilianza mchezo kwa kasi kubwa ya kushambulia huku Coastal ikicheza kwa mikakati ya kujilinda ili isiruhusu mabao mengi kama ambavyo iliwatokea katika mchezo wa nusu fainali ilipochapwa mabao 5-2 dhidi ya Azam FC, Uwanja wa New Amaan Complex Visiwani Zanzibar Agosti 8.

Licha ya Simba kushambulia kwa kasi na kupata bao la utangulizi dakika ya 10, kupitia kwa Saleh Karabaka ila nyota wa kikosi hicho walikosa utulivu wa kumalizia pasi  za mwisho za kufunga.

Miongoni mwa nyota hao ni mshambuliaji mpya, Steven Mukwala ambaye alipata nafasi ya wazi dakika ya 19 na kushindwa kufunga huku akikosa utulivu ambao ungeweza kuiwezesha timu hiyo kuongoza kwa idadi kubwa ya mabao katika kipindi kwanza.

Ukosefu wa utulivu kwa Simba ulimfanya kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids kuonekana wazi kumkera.

Kwa upande wa Coastal Union inayonolewa na Kocha Mkenya, David Ouma ilianza taratibu na hadi iliporuhusu bao la kwanza ndipo ilipoanza kushambulia, huku ikitengeneza nafasi mbili za wazi ambazo hata hivyo hawakuweza kuzitumia vizuri wakiongozwa na mshambuliaji wa timu hiyo, John Makwatta.


Wasikie makocha

Kocha wa Coastal, Ouma alisema aliwasoma Simba kipindi cha kwanza walichokitawala na kipindi cha pili waliziba mianya iliyowapa nafuu na pia walipoteza nafasi ya wazi na kukisifia kikosi hicho huku akisema timu hiyo inaendelea kujengekea na walipata kipimo kizuri kwa mechi za kimataifa ikitarajiwa kucheza na Bravo ya Angola.

"Ni kipimo kizuri na tunaendelea kujipanga kwa mechi zilizopo mbele yetu, kwani bado naitengeneza timu na wachezaji wanaendelea kuimarika zaidi," alisema Ouma raia wa Kenya.

Huku kocha wa Simba, Fadlu, alisema kazi kubwa anayoifanya kwa sasa ni kuifanya Simba ishinde mfululizo na sio mechi moja na kwamba ana kazi kubwa ya kufanya ili wachezaji wake waweze kutumia vizuri nafasi wanazopata.

"Tumemaliza maandalizi ya msimu, lakini bado tunatakiwa kufanya kazi kubwa ya kutumia nafasi za kufunga tunazopata, kama mchezo huu tungekuwa makini nafikiri tulikuwa tunaweza kushinda hata mabao matano, lakini bado tunarudi mazoezini kufanyia kazi makosa hayo," alisema kocha huyo ambaye mara kwa mara alikuwa akihimiza wachezaji wake.


Kikosi chabadilika

Katika mchezo huo, kocha wa Simba, Fadlu Davids alipangua kikosi katika nafasi nne kulinganisha na kile kilichoanza dhidi ya Yanga na kulala 1-0.

Kocha huyo Msauzi, aliyagusa maeneo mawili tu ya ulinzi na kiungo kwa kuwaweka nje, Shomary Kapombe, Chamou Karaboue, Mzamiru Yassin na Edwin Balua, akitoa nafasi kwa Kelvin Kijili, Abdulrazak Hamza na Augustine Okajepha na Saleh Karabaka aliowaanzisha.

Licha ya kuwa na uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni, Hamza aliyetokea Supersport United ya Afrika kusini atatumika kama beki wa kati akicheza sambamba na Che Malone na kuonyesha kiwango cha juu.

Kijili ambaye alingia kipindi cha pili katika dabi dhidi ya Yanga, aliendelea kutumika upande wa beki ya kulia huku kushoto akisalia nahodha wa kikosi hicho, Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Viungo wa kati ni Okajepha na Debora Fernandes ambao walicheza pamoja kipindi cha pili katika dabi, mawinga ni Karabaka na Joshua Mutale huku Jean Charles Ahoua na Steven Mukwala wakiongoza mashambulizi ya wekundu hao wa Msimbazi.


Coastal watano

Kwa upande wa kocha wa Coastal Union, David Ouma alifanya mabadiliko ya wachezaji watano tofauti na wale walianza siku walipopokea kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa Azam FC akiwapiga benchi kipa Athuman Msekeni na kumuanzisha Ramadhan Chuma pamoja na kuwaacha Felly Mulumba, Gerson Gwalala, Gift Abubakar na Abdalla Hassan na kuwaanzisha, Ramadhani Idd, Lukas Kikoti, Abdallah Denis na Denis Modzaka.