Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba na mtihani wa kumaliza kinara Kundi A

Simba Pict

Muktasari:

  • Simba itakuwa wenyeji wa Constantine katika mechi ya mwisho ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku kila moja ikisaka ushindi kwa nia ya kutaka kumaliza kileleni mwa msimamo, lakini nyota wa Wekundu wamesisitiza hakuna namna yoyote leo Kwa Mkapa ila kupata ushindi na kumaliza kibabe.

NI kweli Simba itashuka uwanjani jioni hii bila mashabiki, lakini mastaa wa timu hiyo wameipiga mkwara CS Constantine ya Algeria leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, haichomoki kwani wanataka kulipa kisasi ya kipigio cha 2-1 ilichopewa ugenini, lakini kutaka kumaliza kibabe mechi ya Kundi A.

Simba itakuwa wenyeji wa Constantine katika mechi ya mwisho ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku kila moja ikisaka ushindi kwa nia ya kutaka kumaliza kileleni mwa msimamo, lakini nyota wa Wekundu wamesisitiza hakuna namna yoyote leo Kwa Mkapa ila kupata ushindi na kumaliza kibabe.

Mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, Simba inahitaji wa lazima ushindi ili kumaliza kinara wa Kundi A kwa kufikisha pointi 13 na kuiacha CS Constantine nafasi ya pili na pointi zake 12 ilizonazo sasa.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amefichua katika mchezo wa leo watacheza soka lao walilozoea huku malengo yao ni kushinda, huku akiamini watakutana na ugumu mkubwa kutoka kwa wapinzani wao wanaohitaji sare tu kulinda nafasi yao.

SIM 01

"Haiwezi kuwa mechi rahisi kwa kuwa tunahitaji kushinda ili kuongoza kundi na wenzetu wanahitaji hata alama moja, lakini hatuna presha, tutacheza soka letu tulilozoea," alisema Fadlu na kuongeza.

"Ni muhimu kwetu kumaliza hatua ya makundi tukiwa vinara, kwa sababu hii itatuepusha na baadhi ya timu kubwa kama Zamalek ambao ni wana uzoefu mkubwa, lakini hata Al Masry hivi sasa inafanya vyema na inaonekana ni timu ngumu na yenye nguvu sana, lakini kama unataka kushinda mashindano haya lazima uwe tayari kujiandaa na kufanya mambo yawe rahisi kwako.

"Kumaliza kundi ukiwa wa kwanza hii itafanya mambo kuwa rahisi kwetu katika hatua inayofuata. Ukiangalia kwa sasa timu yoyote itakayokutana na Simba itapambana kujaribu kushinda iwe ya kwanza au ya pili katika kundi, hivyo kuna ugumu."

SIM 02

Wakati kocha Fadlu akiyasema hayo, wachezaji wa Simba wakiongozwa na nahodha Mohammed Hussein 'Tshabalala' na Jean Charles Ahoua kwa nyakati tofauti wamesisitiza 'Watawaonyesha Constantine' kwani wanataka ushindi ili wamalize vinara wa kundi hilo.

Ukiangalia mpaka sasa kabla ya mechi za leo, timu tatu zinaongoza makundi mengine matatu ya mashindano hayo na mbili zimejihakikishia kumaliza zikiwa vinara huku moja ikiwa na nafasi kubwa ya kufanya hivyo.

Mbili ambazo zimeshajihakikishia kuongoza makundi ni RS Berkane ya Morocco ambayo hata ikipoteza leo ikiwa nyumbani dhidi ya Stellenbosch itaendelea kusalia kileleni mwa Kundi B, kwani ina pointi 13 na ilihali wapinzani wao wana tisa, pia kuna Zamalek iliyojihakikishia uongozi wa Kundi D baada ya kukusanya pointi 11 huku inayofuatia ikiwa na pointi sita.

SIM 03

USM Alger ina nafasi kubwa ya kumaliza ikiwa kinara wa Kundi C, kwani hadi sasa ina pointi 11 na mechi ya mwisho itakuwa nyumbani ikicheza na ASC Jaraaf ambayo ina pointi nane.


REKODI ZA VIGOGO HAO

Zamalek imewahi kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili ambazo ni msimu wa 2018/2019 na msimu uliopita 2023-2024 ambazo zote hizo iliichapa RS Berkane.

Timu hiyo ya Misri, katika michuano ya CAF ina rekodi ya kubeba jumla ya mataji 13. Mbali na mawili ya Kombe la Shirikisho, pia inayo matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochukua mwaka 1984, 1986, 1993, 1996 na 2002. CAF Super Cup (5) na African Cup Winners' Cup (1) michuano ambayo kwa sasa haipo kwani mwaka 2004 iliunganishwa na Caf Cup ikazaliwa Kombe la Shirikisho.

SIM 04

USM Alger imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho mara moja ambayo ni msimu wa 2022/2023 ilipoifunga Yanga. Pia ina taji moja la Caf Super Cup ililobeba mwaka 2023 huku mwaka 2015 ikishika nafasi ya pili katika Ligi ya Mabingwa.

RS Berkane imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara mbili, msimu wa 2019/2020 na 2021/2022, pia ina taji moja la CAF Super Cup ililoshinda mwaka 2022. Kuanzia msimu wa 2018–19 hadi sasa timu hiyo kutoka Morocco ina rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho mara nne jambo linaloashiria kuwa ipo imara.

Rekodi zinaonyesha, msimu wa 2018–19 RS Berkane ilishika nafasi ya pili ikipoteza fainali kwa kufungwa penalti 5–3 na Zamalek. Baada ya kukosa ubingwa msimu huo, 2019–20 ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Pyramids bao 1-0, kisha msimu wa 2020-21 iliishia makundi na 2021–22 ilibeba ubingwa kwa ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Orlando Pirates.

SIM 05

RS Berkane katika msimu wa 2022-23 iliishia mtoano, wakati msimu wa 2023–24 ilimaliza nafasi ya pili baada ya kupoteza fainali mbele ya Zamalek kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2. Ilianzia nyumbani ikashinda 2-1, Zamalek ikaenda kumaliza kazi kwao kwa kushinda 1-0.

Ikumbukwe pia Simba katika mara tano tofauti ilizowahi kushiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika, ni mara moja tu imewahi kumaliza ya kwanza kwenye kundi hivyo msimu huu itakuwa ni mara ya pili ikiwa itafanikiwa kufanya hivyo.

Mara moja pekee ambayo Simba iliwahi kuongoza kundi ni msimu wa 2020/2021 na ilikuwa ya kwanza kwenye kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika ikikusanya pointi 13 na nyuma yake kulikuwa na Al Ahly iliyokuwa na pointi 11.


SIM 06

UGUMU WA MCHEZO

Constantine walionyesha umwamba wao wakiwa nyumbani katika mchezo wa kwanza dhidi ya Simba na kushinda 2-1 licha ya kutanguliwa bao 1-0 kipindi cha kwanza lililofungwa na Mohamed Hussein.

Kipindi cha pili iliwachukua takribani dakika tano kupata mabao mawili yaliyowapa ushindi huo, ilianza dakika ya 46 Abdulrazack Hamza alijifunga kisha Brahim Dib akaweka la ushindi dakika ya 50.

Kupoteza mbele ya Constantine ni kitu kinachowauma zaidi Simba kwani mchezo huo pekee hadi sasa ndiyo hawakuondoka na pointi yoyote katika kampeni yao ya michuano hiyo msimu huu.

Ukiangalia kuanzia mtoano, ilianza na 0-0 dhidi ya Al Ahli Tripoli, kisha nyumbani ikaipa 3-1 ikafuzu makundi ambapo nyumbani ilizifunga Bravos 1-0 na CS Sfaxien 2-1. Ugenini ikafungwa 2-1 na CS Constantine, ikashinda 1-0 mbele ya CS Sfaxien na 1-1 kwa Bravos.

Wachezaji wa Simba wanataka kulipiza kisasi katika mchezo wa leo kwa kuifunga CS Constantine na kuweka rekodi ya ushindi kwa asilimia 100 nyumbani kimataifa msimu huu.

Kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara ambaye amedaka mechi zote za kimashindano kikosini hapo msimu huu, amesema: "Hatusahau kwamba hii ni timu iliyotufunga ugenini, hakuna timu nyingine iliyoondoka na pointi tatu dhidi yetu, tunataka kusahihisha makosa yetu, walipata ushindi ule kwa makosa yetu, tutakuwa nyumbani kusahihisha makosa yetu."

Simba katika mechi zao tatu za Kombe la Shirikisho Afrika ilizocheza msimu huu kuanzia mtoano, mpinzani wake alipojaribu kupishana naye alipata wakati mgumu.

Hiyo inaonyesha wazi Simba inapocheza nyumbani, suala la kujilinda zaidi kwao sio kipaumbele zaidi ya kushambulia muda wote na imempa matokeo mazuri hata pale hali inapokuwa ngumu.

Katika mechi dhidi ya Al Ahli Tripoli, Simba ilianza kuruhusu bao, lakini ikakaa imara na kusawazisha, ikaongeza na kufunga lingine ikashinda 3-1.

Mbele ya Bravos, wapinzani walionekana kuwa wagumu, kosa moja tu likawagharimu walipocheza faulo kwenye boksi, Jean Charles Ahoua akafunga kwa penalti kabla ya CS Sfaxien nao kutangulia kwa bao la mapema dakika ya tatu, Kibu Denis akaisawazishia Simba dakika ya saba. Wakati ikiaminika mechi inaisha kwa sare, Kibu akafunga bao la ushindi dakika ya 90+8.

Wakati Simba ikicheza soka la kushambulia muda mwingi ikiwa ni silaha yao ya nyumbani, CS Constantine wanapokuwa ugenini wanacheza kwa kuvizia ukizingatia mchezo wa leo kwao sare ni faida kubwa hivyo itawavuta wapinzani wao na kuwashambulia kwa kushtukiza. Simba inapaswa kuwa makini na hilo.


MWAMUZI KUTOKA MSUMBIJI KUAMUA

Celso Armindo Alvação ambaye ni mwamuzi kutoka Msumbiji anayesifika kwa kumwaga kadi kama njugu, mbali na kutoa penalti ndiye atapuliza filimbi katika mchezo huo wa leo. Atasaidiwa na waamuzi pia kutoka Msumbiji.

Rekodi za Alvacao zinaonyesha mwamuzui huyo katika mechi 21 za kimataifa alizochezesha amemwaga jumla ya kadi 83 ikiwa ni wastani wa kadi nne kwa kila mchezo, huku za njano zikiwa ni 81 na nyekundu mbili.

Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa na kismati na wenyeji kushinda kwani katika michezo hiyo 21, tisa timu wenyeji imeshinda, huku sita ikiwa ni kwa wageni kuibuka na ushindi na nyingine kama hizo zikiisha kwa sare.

Katika mechi tano zilizopita za kimataifa zikiwamo tatu za kufuzu za Afcon 2025 na mbili za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, ametoa jumla ya kadi za njano 15 kuonyesha, hana huruma kumwaga kadi kwa wachezaji wanaozingua uwanjani.