Simba Asec, Wydad vitani Kombe la Shirikisho

Dar es Salaam. Timu ya Simba inatarajia kukutana na upinzani mkubwa kwenye michuano ya Kombe la Shrikisho Afrika baada ya vigogo wengi kuangukia huko.
Simba ambayo imekuwa maarufu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa miaka kadhaa sasa, imemaliza msimu wa Ligi Kuu Bara katika nafasi ya tatu jambo linaloilazimisha kushiriki michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika.
Hadi sasa, tayari timu hiyo imeshaonyeshwa kuwa itakutana na upinzani mkubwa tofauti na jinsi ambavyo mashabiki walikuwa wakitarajia awali kuwa mashindano hayo yatakuwa mepesi kwa timu yao na itakuwa nafasi ya pekee kwenda mbali zaidi ya robo fainali, hatua ambayo wameishia kwa misimu mitano kwenye michuano ya Caf.
Timu za kongwe za Wydad Club Athletic ya Morocco inayoshika nafasi ya tatu kwa ubora Afrika, Asec Mimosas ya Ivory Coast inayoshika nafasi ya 14, As Vita ya Congo zitacheza kwenye michuano hiyo msimu ujao baada ya kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa kama kawaida yao kwa misimu kadhaa iliyopita.
Wydad, Asec Mimosas na AS Vita pamoja na Simba ni kati ya timu ambazo zimekuwa zikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mfululizo kwa miaka ya hivi karibuni, hivyo kitendo cha kutua kwenye shirikisho kinaonyesha kuwa zinakwenda kutoa upinzani mkali kwa Simba.
Hata hivyo, bado kuna uwezekano mkubwa timu moja kigogo kutoka nchini Misri aidha, Al Ahly ambayo ni timu namba moja kwa ubora Afrika ikiwa ndiyo bingwa wa Ligi ya Mabingwa, Zamalek au Pyramids moja wapo ikaangukia kwenye michuano hii.
Misri itafanikiwa kuingiza timu nne kwenye michuano ya Caf msimu huu na mbili kati ya hizo zitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Hadi sasa Ligi Kuu ya nchi hiyo haijamalizika huku Pyramids ikiwa kileleni baada ya kucheza michezo 22 na pointi 53, Ahly ipo nafasi ya nane ikiwa imeshacheza michezo 15 na pointi 33, Zamalek ambayo ni mabingwa watetezi wa michuano hii ipo nafasi ya 12, pointi 28 ikicheza michezo 17 kwenye ligi hiyo yenye timu 18.
Hii inaonyesha kuwa Simba ambayo mara yake ya mwisho kufuzu kucheza michuano hii ilikuwa msimu wa 2021/2022, ikianzia hatua ya mtoano ambapo alikwenda hadi hatua ya robo fainali na kutolewa na Orlando Pirates kwa penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 itatakiwa kuwekeza nguvu kama inataka kufika mbali.
Timu hizo vigogo ambazo zimefuzu kwenye hatua hiyo hadi sasa zina historia na Simba, ambapo msimu uliopita ilikuwa kundi moja na Asec Mimosas kwenye Ligi ya Mabingwa.
Katika michezo minne ya Simba dhidi ya Asec kila mmoja imeshinda mchezo mmoja na zimetoka sare michezo miwili, huku dhidi ya Wydad Simba ikishinda miwili na Wydad miwili.
Kwenye michezo dhidi ya Vita kumbukumbu kubwa ambayo Simba inayo ni kichapo cha mabao 5-0 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, uliopigwa Januari 19, 2019, lakini ndiyo mchezo pekee iliyoshida dhidi ya Mnyama mingine yote mitatu ikipoteza.
Akizungumzia hatua hivyo, kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema wamekuwa wakifanya maandalizi sahihi kwenye kila hatua na michuano wanayoshiriki hivyo hata huku watajiandaa vyema.
“Ligi ndiyo imemaliza tupo mapumzikoni kidogo, lakini baada ya muda tutarejea kujiandaa na michuano yote ambyo ipo mbele yetu, vizuri ni kwamba huwa tunajiandaa vyema kwenye kila hatua.
“Hata kwenye michuano hii mashabiki waamini kuwa tutakuwa imara kuhakikisha tunatimiza malengo yaliyowekwa,” alisema Matola kiungo wa zamani wa Simba.