Simba, Azam kivumbi leo

Muktasari:
- Hesabu kubwa za Simba ni kusaka pointi tatu zitakazoisadia kupata nafasi ya pili kwenye ligi, inayowaniwa pia na Azam FC ambayo nayo itakuwa uwanjani leo dhidi ya JKT Tanzania ugenini.
Simba inarudi uwanja wa nyumbani leo, itakapowakaribisha Geita Gold, kwenye mchezo mgumu ambao kila timu itakuwa na hesabu zake zikielekea kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara.
Hesabu kubwa za Simba ni kusaka pointi tatu zitakazoisadia kupata nafasi ya pili kwenye ligi, inayowaniwa pia na Azam FC ambayo nayo itakuwa uwanjani leo dhidi ya JKT Tanzania ugenini.
Simba na Azam, zote zina pointi 60 kwenye ligi lakini matajiri hao wa Chamazi wako nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, timu hizo mbili zikiendelea kufukuzana kuwania nafasi ya pili itakayowapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Wakati Simba ikipambana kutafuta nafasi ya pili, Geita yenyewe itakuwa uwanjani ikitaka ushindi ili kuepuka na dhahama ya kushuka daraja, ikiwa inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 27 ikibakiza mechi tatu kumaliza msimu.
Rekodi zinaibeba Simba mbele ya Geita kwani kwenye mechi tano ilizokutana, imeshinda nne na kutoa sare moja.
Simba inayofundishwa na kocha Juma Mgunda, imekuwa na mwendo mzuri kuanzia iwe chini ya mzawa huyo ikiwa haijapoteza mchezo wowote kati ya sita iliyocheza, imeshinda minne na kutoka sare miwili.
Mshambuliaji Freddy Michael Kouablan, atakuwa na dakika 90 zingine zitakazompa nafasi ya kuendeleza moto wake wa mabao akiwa tayari ameshafunga sita yaliyorudisha kasi yake ya kufumania nyavu.
Kuelekea mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1:00 jioni, Mgunda amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi.
"Maandalizi ya mchezo huu yamekamilika, tunafahamu kwamba tunakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Geita, wanahesabu zao na sisi tuna zetu, hii ni timu yenye wachezaji wazuri na kocha mzuri kwa hiyo mashabiki wetu waje uwanjani kuwapa nguvu wachezaji wao," alisema Mgunda.
Tangu Geita iwe chini ya kocha Denis Kitambi imecheza mechi 15 ikishinda mbili pekee na kupoteza saba huku ikitoa sare sita ambapo imeendelea kuwa na matokeo yanayotia mashaka.
Changamoto kubwa inayoitafuna ni ubutu wa safu yake ya ushambuliaji ambayo haijafunga bao lolote kwenye mechi tano zilizopita ambapo mara ya mwisho kupata bao ilikuwa Aprili 13,2024, ilipolazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar.
"Kubwa ni kwamba katika maisha yangu ya soka ni mara ya kwanza nakwenda kwenye mechi kubwa bila kuangalia ubora wa mpinzani na sijafanya hivyo kwa sababu soka ni mchezo wa wa magoli na sisi hatufungi, kwa hiyo tumejikita kuwapa mbinu vijana wetu ili waweze kutumia nafasi wanazotengeneza,"alisema Kitambi.
Azam kazi ipo
Baada ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Azam FC leo itakuwa ugenini ikikaribishwa na JKT Tanzania kwenye mchezo utakaopigwa Meja Isamhyo, huku timu zote zikiwa na presha kubwa.
Azam iko kwenye ushindani mkubwa na wapinzani wao Simba ambao wanalingana pointi kwa sasa kwani katika mechi 27 walizocheza wawili hao wote wana jumla ya pointi 60, zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufunga.
Azam inaanza wiki na maafande hao kwa hesabu kali za kutotakiwa kuruhusu mabao katika mechi hiyo ya 28 ili kuendelea kujiweka katika mikono salama ya kupata nafasi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Kwa Maafande nako hali si shwari, kwani wako nafasi ya tisa wakiwa wamecheza mechi 27 sawa na wapinzani wao, wataingia katika mechi hiyo wakiwa na kibarua cha kulinda nafasi yao kwani bado hawapo salama wakiwa na pointi 31 tofauti ya pointi mbili tu na timu inayoweza kucheza nafasi ya mtoano kwenye ligi.