Serikali ilivyomlinda Morocco Taifa Stars
Muktasari:
- Kabla ya kutolewa na Morocco katika robo fainali, Taifa Stars ilimaliza ikiwa kinara wa kundi B la fainali za CHAN ambapo ilikusanya pointi 10
Dar es Salaam. Licha ya Taifa Stars kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024, Serikali imelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuendelea kulipa muda benchi la ufundi la lenye idadi kubwa ya wazawa kwa vile limeipa mabadiliko chanya na mafanikio makubwa.
Taifa Stars iliaga fainali za CHAN 2024 juzi Ijumaa baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hata hivyo hatua hiyo ndio ya juu zaidi kwa Taifa Stars kufika katika fainali hizo kwani awamu mbili zilizopita ambazo ni 2009 na 2020 iliishia katika hatua ya makundi kama ilivyo katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo mara tatu ilizowahi kushiriki haikuwahi kuingia hatua ya mtoano.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa kilichoonyeshwa na Taifa Stars katika fainali za CHAN 2024 ni matunda ya kazi nzuri za benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco' hivyo linapaswa kupewa muda zaidi wa kuendelea kuinoa timu hiyo.
“Tumefika mahali tumeanza kujitambua kwamba tunao walimu wazuri wa ndani. Tumefika hatua nzuri chini ya walimu wazawa na sasa tunaona wachezaji wetu, hatua nzuri waliyofikia. Walimu bado wataendelea kutunzwa na shirikisho waendelee kuweka programu zao. Tunataka tuendelee kucheza mashindano mengi zaidi.
“Walimu wamethibitisha kwamba tunao uwezo kwa walimu wazawa. Hawa waendelee kuimarishwa, waendelee kuweka program za kisasa za baadaye. Badala ya kuwa wanabadilishwa badilishwa. Wameonyesha umoja wameonyesha mafanikio kwa hatua waliyofikia.
"TFF wapeni nafasi ya kuendelea hapo wanapoona sasa wanafaa kwenda kwa sababu na wao wamekuwa wakijifunza pia,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema kuwa serikali imeridhishwa na kiwango ambacho Taifa Stars imekuwa ikikionyesha na inaamini itapata mafanikio makubwa siku za usoni.
“Sisi wanamichezo tunajua kanuni zetu kwenye michezo tunakwenda kushinda, kutoka suluhu au kupoteza mchezo lakini kwa mazingira yapi na timu ipi hayo yote tunayalinganisha na kuja hapa kuwapa hongera.
“Wachezaji wetu na walimu wa timu, Watanzania wameanza kuona mabadiliko ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini kutoka klabu mpaka timu za taifa. Tumefika hatua nzuri na tunaendelea kujipima na hii CHAN ni kipimo kizuri sana kwetu.
“Niwahakikishie wachezaji, bado mna nafasi kubwa na nzuri ya kufanya vizuri huko mbele. Naamini baada ya michezo hii, shirikisho litaendelea kuifanya timu ya taifa kuwa na mashindano mengi ya mazoezi ya kirafiki ili kuwaimarisha wachezaji wetu," amesema Majaliwa.
Kabla ya kutolewa na Morocco katika robo fainali, Taifa Stars ilimaliza ikiwa kinara wa kundi B la fainali za CHAN ambapo ilikusanya pointi 10 katika mechi nne, ikifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja.