Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saka anavyomuumiza kichwa Arteta

Muktasari:

  • Saka ambaye amekuwa mchezaji muhimu zaidi kwa Arsenal, ameumia misuli ya paja wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace ambao Arsenal ilishinda 5-1.

London, England. Ishu ya Bukayo Saka kuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki tatu inafahamika, ishu mpya inayozungumzwa kwa sasa ndani ya Arsenal nani atakuwa mbadala wake huku kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta akiumiza kichwa katika hilo.

Saka ambaye amekuwa mchezaji muhimu zaidi kwa Arsenal, ameumia misuli ya paja wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace ambao Arsenal ilishinda 5-1.

Kama mashabiki wa Arsenal ukiwauliza wachague mchezaji ambaye watapenda acheze msimu mzima bila ya kuumia, basi Bukayo Saka angekuwa wa kwanza au wa pili kwenye orodha hiyo.

Saka amehusika kwenye mabao 15 katika Premier msimu huu akifunga matano na asisti kumi, ndiye mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi kikosini hapo ikiwa ni kwa asilimia 45.5.

Tangu msimu wa 2020-2021, Saka ameitumikia Arsenal kwa dakika 12,950 zikiwa ni nyingi zaidi kwa wale wanaocheza eneo la mbele akifuatiwa na Gabriel Martinelli (8,238), huku Kai Havertz ambaye huu ni msimu wa pili kikosini hapo akicheza kwa dakika 4,031, Gabriel Jesus ni dakika 3,908.

Wakati huu ambao Saka yupo nje, Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anahitaji kutafuta mbadala sahihi ili kuendelea kupambania malengo yao.

Umuhimu wa Saka kikosini hapo unafahamika kwani nyota huyo anayecheza zaidi upande wa kulia eneo la kushambulia katika misimu mitatu iliyopita, amekosa mechi kumi tu kati ya 172 za mashindano yote kikosini hapo. Tangu ameanza kucheza Premier League miaka sita iliyopita, hakuwahi kukosa zaidi ya mechi moja kwa sababu ya majeraha.

Kati ya wachezaji watatu wa mbele wa timu hiyo katika misimu minne iliyopita, Saka ana dakika nyingi zaidi. Sio tu kwamba yeye ni mmoja wa wapiga kona wakuu wa Arsenal pamoja na Declan Rice, lakini jinsi timu hiyo inavyotengeneza mashambulizi yake asilimia kubwa yanapitia eneo la Saka.

Kwa msimu huu, Arsenal imeitumia upande wa kulia anapocheza Saka kufanya mashambulizi kwa asilimia 46, huku kushoto kwa Martinelli ni asilimia 33, pale kati asilimia 21.

“Ni mchezaji mkubwa kwetu, hivyo lazima tuone umuhimu alionao kwenye timu. Ninaweka mambo sawa, nitazungumza na vijana wangu kuona ni jinsi gani tutacheza bila ya uwepo wake huku tukilichukulia jambo hilo kwa njia chanya. Hivyo ni wazi tutakuwa tofauti,” alisema Arteta kuhusu Saka.

Kabla ya Saka kuumia, wiki sita za mwanzoni mwa msimu huu Arsenal ilimpoteza nahodha wake Martin Odegaard kutokana na majeraha lakini Arteta hakusema kama watabadili aina ya kutengeneza mashambulizi mpaka amerejea.

Lakini kwa Saka ni tofauti hasa ukiangalia winga wa kulia wa timu hiyo Raheem Sterling pia alikaa nje ya uwanja akiuguza majeraha.


Nani mbadala wake?

Gabriel Martinelli huu ndio wakati wake kuchukua nafasi hiyo na kufanya makubwa licha ya kwamba yeye ni mzuri zaidi akitokea kushoto. Baada ya Saka kuumia, Martinelli akaenda kucheza upande huo kwenye ushindi wa 5-1 dhidi ya Palace, akifunga bao na kutoa pasi ya bao.

Gabriel Jesus pia amewahi kucheza upande wa kulia, akianza katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester City mwaka jana wakati Saka alipokosekana. Ingawa kwa sasa Jesus anafanya vyema kama mshambuliaji wa kati, Arteta anaweza kuamua kubadilisha nafasi yake ili kuziba pengo la Saka.

Tatizo ni kwamba Martinelli na Jesus wote ni wachezaji wanaotumia mguu wa kulia, jambo linalomaanisha kwamba hawatakuwa tishio kama Saka anayetumia mguu wa kushoto.

Kai Havertz ni mchezaji mwingine ambaye Arteta ameonyesha kuwa anafikiria kumtumia upande wa kulia. Hata hivyo, Havertz amezoea kucheza kama mshambuliaji wa kati, uwezo wake wa kushinda mipira ya juu unaweza kuwa hauhitajiki sana upande wa kulia.

Leandro Trossard ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili, jambo linalofaa kwa nafasi hii. Hata hivyo, Trossard ameonekana kuwa mzuri zaidi akitokea benchi hivyo suala la kucheza kikosi cha kwanza kwake sio kwa kiwango kikubwa.