Prime
Sababu 10 Simba kubeba ubingwa

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amepanga kutumia mbinu ya aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ya kutoa nafasi ya kucheza kwa kundi kubwa la wachezaji, huku akianika sababu za kwanini kikosi chake kitatwaa ubingwa msimu huu.
Miongoni mwa sababu zilitolewa na Robertinho ni pamoja na kuwa na nyota wenye ubora kila eneo, benchi bora la ufundi, ubora wa kambi ya Uturuki, viongozi kufanya usajili makini na ushirikiano wanaopata kutoka kwao.
Akizungumza jana baada ya kuwasili nchini, Robertinho alisema tofauti na msimu uliopita, awamu hii ana kundi kubwa la wachezaji ambao hawapishani sana viwango, jambo linalompa nguvu ya kusaka ubingwa.
"Kwa sasa tuna uwiano mzuri wa kikosi. Kuna wachezaji wapya wenye ubora wa juu, ni jambo la muhimu na napongeza uongozi. Tuna wigo mpana wa kufanya mabadiliko kama unavyofahamu kuna suala la majeraha na pia mabadiliko ya kimfumo.
"Kiwango ambacho kimeonyeshwa na wachezaji kwenye kambi ya maandalizi ni kizuri na kinafurahisha. Tunaweza kutumia wachezaji tofauti tofauti kwenye nafasi mbalimbali kwa vile wana kiwango kinachofanana.
"Kwa mfano nikitaka kucheza kwa kushambulia sitopanga idadi kubwa ya viungo wa ulinzi, lakini tukiwa na mpango wa kulinda maana yake nina namba ya kutosha ya viungo wa ulinzi," alisema.
Kocha huyo alisema kazi kubwa ambayo wameifanya katika kambi ya Uturuki ni kutengeneza uhusiano mzuri wa wachezaji ndani na nje ya uwanja, wakiamini utakuwa ni chachu kwao kufanya vyema.
"Tunahitaji kutimiza malengo ya kufanya vizuri msimu ujao kwa kutwaa ubingwa. Tunahitajika kuwa na timu nzuri na kabla hujawa nayo, unapaswa kuifanya iwe familia na ndicho ambacho tumekifanya.Sasa tuna makundi mawili (timu), ambayo yote tunaweza kuyatumia. Kumbuka tuna mashindano muhimu mengi mbele. Tuna tamasha la Simba Day, ambayo yote tumeweka malengo ya kufanya vizuri. Kuhusu nani atacheza itategemea na ufanisi na mchango wa kila mmoja ndani ya uwanja,"alisema Robertinho.
Simba imefanya usajili wa nyota tisa wapya ambao ni Willy Onana, Che Fondoh Malone, David Kameta, Fabrice Luamba Ngoma, Hussein Kazi, Hamis Abdallah, Shaban Chilunda, Luis Miquissone na Aubin Kramo.
Usajili wa Malone na Kazi unafanya iwe na mabeki wanne wa kati wakiungana na Henock Inonga na Kennedy Juma wakati ingizo la Kameta linafanya iwe na mabeki wawili wa kulia pamoja na Kapombe, huku Israel Mwenda akihamishwa kwenda nafasi ya beki wa kushoto kusaidiana na Mohammed Hussein 'Zimbwe'.
Ingizo la Ngoma linalipa benchi la ufundi la Simba machaguo matatu katika nafasi ya kiungo wa ulinzi, akiungana na Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute, wakati Onana anafanya iwe na viungo wawili washambuliaji akiwa na Clatous Chama.
Katika nafasi ya winga wapo Kramo, Miquissone, Mwanuke, Saido Ntibazonkiza na Kibu Denis, wakati nafasi ya mshambuliaji wa kati ni John Bocco, Jean Baleke na Mohammed Musa.