Saadun: Msimu umekuwa bora kwangu

Muktasari:
- Saadun amejiunga na Azam FC akitokea Geita Gold inayoshiriki Championship. Tangu ametua kikosini hapo chini ya makocha wawili tofauti waliomfundisha ameweza kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza.
“Huu ni wakati wangu, lilikuwa ni suala la muda na mimi kufanya hiki ninachokifanya baada ya kurudi kucheza Tanzania.
“Kila kitu ni muda. 2024/25 kwangu ni bora kwani nimerudi lakini msimu huu ndio nimekuwa bora na nakiri kuwa huu ni wakati wangu,” ni maneno ya Nassoro Saadun mshambuliaji wa Azam FC katika mahojiano yake na Spoti Mikiki.
BAO BORA
Mshambuliaji huyo ambaye hana rekodi nzuri tangu amerejea Ligi Kuu Bara ya kufunga mabao mengi kama alivyofanya msimu huu amesema kuwa kati ya mabao sita aliyofunga msimu huu, aliloweka kimiani kwenye mechi dhidi ya KMC iliyochezwa Septemba 19 mwaka jana ndio bora zaidi.
“Nimefunga mabao sita yote ni mazuri kwa sababu yaliingia nyavuni lakini bao langu bora ni dhidi ya KMC ambalo ndio lilikuwa bao la kwanza tangu nimejiunga na timu hii,” anasema na kuongeza;
“Ni bora kwa sababu ni nadra kufunga mabao ya aina ile nikiwapunguza mabeki hadi kipa na kukwamisha mpira nyavuni hivyo kwangu kati ya sita niliyofunga hilo ndio bora.”
DABO/TAOUSSI
Saadun amejiunga na Azam FC akitokea Geita Gold inayoshiriki Championship. Tangu ametua kikosini hapo chini ya makocha wawili tofauti waliomfundisha ameweza kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza na mwenyewe amezungumzia kuhusu hilo.
“Nafurahi nimepata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza chini ya makocha wote wawili Yosouph Dabo ambaye aliondoka mwanzoni mwa msimu na sasa Rachid Taoussi kwani naamini ni kujituma na kuonyesha nini nakihitaji mazoezini ndio siri kubwa,” anasema Saadun
Kujituma na kuamini katika kipaji ndio siri ya mafanikio aliyonayo licha ya changamoto za kucheza nafasi moja na wachezaji wazoefu.
“Nafasi yangu naiona mbali na siwezi kubweteka kwa kidogo ninachokipata naamini msimu huu utakuwa bora kwangu kwani tayari nimefikia nusu ya malengo yangu. Siwezi kusema nina malengo gani kwani sipendi kujipa presha mwenyewe lakini naamini nitatumia kila nafasi ninayopewa kuhakikisha naipambania timu na malengo yangu binafsi,” anasema Saadun.
Anasema familia yake imekuwa wakimpa sapoti ya kutosha hasa wakiwa na mechi za nyumbani ambazo wamekuwa wakijaa uwanjani na kumpa nguvu.
Mchezaji huyo anafichua kuwa ana mahusiano mazuri na kocha Taoussi ambayo yana faida kwa upande wake.
“Kwa sasa nikiwa na Taoussi nahisi nafanya kazi na baba yangu kama ninavyo muita huwa simuiti kocha namuita baba kwa sababu amekuwa kiongozi sahihi kwangu na kuhusu lugha naelewana naye vizuri licha ya mimi kushindwa kumjibu,” anasema Saadun.
PRESHA ILIKUWA KUBWA
Usajili wake kutua Azam FC ulizua maswali mengi kwa wadau wa soka wakiamini hakuna atakachokifanya kutokana na rekodi yake Geita Gold kutokuwa nzuri lakini ameweza kuwa nyota wa kutumainiwa kikosi cha kwanza mwenyewe amefunguka siri ya hayo.
“Haikuwa rahisi kwa sababu presha ilikuwa ni kubwa sana lakini namshukuru Mungu nimeweza kuingia kwenye mfumo na kuaminiwa na makocha wote wawili walionifundisha kwa nyakati tofauti.
“Azam FC ni timu kubwa baada ya kukutana na wachezaji, kocha na kufanya mazoezi presha ilipungua na niliamini ninauwezo wa kufanya vizuri namshukuru Mungu mambo yanaenda vizuri,” anasema Saadun.
FEI TOTO NI BORA AFRIKA
Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni jina linalotajwa na wachezaji wengi misimu ya hivi karibuni na Saadun amefunguka sababu ambazo anaamini kwa nini amekuwa kiungo huyo amekuwa akiimbwa midomoni mwa wachezaji wengi wanaocheza ligi.
“Nacheza Azam FC nimekutana na wachezaji wengi na kufanya nao kazi lakini nafurahi zaidi nikicheza sambamba na Fei Toto eneo la ushambuliaji kwa sababu ni mchezaji bora Afrika na kila mchezaji anatamani kucheza naye.
“Fei Toto sio mchezaji bora Tanzania tu nafikiri ni Afrika nzima kucheza naye kwa upande wangu nakuwa na utulivu mkubwa na nafurahi kwa sababu anarahisisha vitu vingi uwanjani,” anasema mchezaji huyo.
MIKWALA YA MABEKI
Washambuliaji huwa wanakutana na ugumu kutoka kwa mabeki hasa wanapoenda kushambulia lango la wapinzani kama ambavyo anafunguka Saadun.
“Mabeki wana maneno ya kukera ukiondoa changamoto ya kukanyaga, kupiga ambayo inafanywa kwa siri kubwa bila ya waamuzi kuona ni nadra sana makosa kama haya kuonekana ukiondoa hilo pia wana maneno makali ambayo siwezi kuyaweka wazi,” alisema Saadun.