Rudiger hatihati kuitwa timu ya taifa

Muktasari:
- Licha ya mchezaji huyo kuomba radhi kupitia mitandao ya kijamii kwa kile alichokifanya katika mchezo huo bado shirikisho la soka Hispania halijasema chochote kuhusu hatma yake.
Mkurugenzi mtendaji wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Ujerumani, Rudi Völler amechukizwa na kitendo cha utovu wa nidhamu alichokionyesha Antonio Rudiger katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mfalme (Copa del rey) dhidi ya Barcelona.

Akizungumza na shirika la habari la Dpa siku ya Jumatatu, Völler ambaye alikuwa mshambuliaji wa Ujerumani amesema kwamba Antonio Rudiger anatakiwa kuonyesha heshima kama wachezaji wengine wa timu ya taifa ya Ujerumani.
“Huwezi kufanya hivyo. Anapaswa kubadilika, nadhani na yeye analijua hilo. Rudiger ni mchezaji wa daraja la juu, lakini kama mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani anapaswa kuonyesha tabia yenye hadhi,” amesema Völler.

Katika mchezo huo ambao Madrid ilipoteza kwa mabao 3-2 ilishuhudiwa refa wa mchezo huo Ricardo De Burgos Bengoetxea akionyesha kadi tatu nyekundu kwa wachezaji wa Real Madrid ambao ni Rudiger, Lucas Vazquez na Jude Bellingham.

Rudiger alionyeshwa kadi nyekundu akiwa benchi baada ya kumrushia mwamuzi kipande cha barafu alichokuwa ameshika mkononi huku akitoa maneno yasiyo ya kiungwana kwa refa huyo baada ya beki wa Barcelona, Eric Garcia kuonekana kumchezea vibaya Mbappe huku mwamuzi akionyesha haikuwa faulo.

Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Dietmar Hamann amelitaka shirikisho la mpira wa miguu la Ujerumani kumpa adhabu beki huyo ikiwemo kumuondoa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani.
“Nafikiri shirikisho la mpira wa miguu linatakiwa kumpa adhabu beki huyu na kumuondoa katika kikosi cha timu ya taifa,” amesema Hamann.
Ujerumani itacheza na Ureno katika nusu fainali ya mashindano ya Ulaya (UEFA Nations League) mchezo utakaochezwa Juni 4 mwaka huu kwenye uwanja wa Allianz Arena.

Licha ya mchezaji huyo kuomba radhi kupitia mitandao ya kijamii kwa kile alichokifanya katika mchezo huo bado shirikisho la soka Hispania alijasema chochote kuhusu hatma yake huku adhabu inayotarajiwa kwa mchezaji huyo huwenda akafungiwa kucheza michezo kuanzia minne hadi 12 kutokana na ukubwa wa kosa alilofanya.

Kwa upande wa Lucas Vazquez na Jude Bellingham wao watakosekana kwenye michezo miwili ya Kombe la Mfalme (Copa del rey) msimu ujao baada ya kupewa kadi nyekundu za moja kwa moja.