Ronaldo azidi kuikimbizia rekodi ya mabao
Muktasari:
- Katika mchezo huo ambao Ureno imeshinda mabao 3-2, Ronaldo amefunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 58.
Lisbon, Ureno. Nyota wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo ameendelea kuikimbizia rekodi ya kufikisha idadi ya kufunga mabao 1000 ya michuano rasmi baada ya kuongeza katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Hungury.
Katika mchezo huo ambao Ureno imeshinda mabao 3-2, Ronaldo amefunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 58.
Ushindi huo umeiwezesha Ureno kufikisha alama sita katika kundi ikiwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu ikibakisha mchezo mmoja mkononi.
Wakati Ronaldo akipambana kuweka rekodi hiyo, staa wa Manchester City, Erling Haaland amefanya umafia wa aina yake kwa kufunga mabao matano katika ushindi wa Norway wa mabao 11-1 dhidi ya Moldova.
Haaland ambaye sasa anakuwa amefunga mabao 48 katika mechi 45 alizocheza akiwa na Norway, katika mchezo huo amefungua kalamu yake ya mabao kwa kufunga bao la pili dakika ya 11, kisha akafanya hivyo tena dakika za 36, 43, 52 na 83.
Serbia ambayo ilikuwa nyumbani imepokea kichapo cha maana kutoka kwa England cha mabao 5-0 ikiwa ndio ushindi wa kwanza mkubwa wa kocha Thomas Tuchel tangu ajiunge na timu hiyo.
Hata hivyo, Serbia imemaliza mechi ikiwa pungufu baada ya beki wa kati Nikola Milenkovic kupata kadi nyekundu dakika 72 ambayo imechangia kuruhusu mabao mawili zaidi kwani dakika tatu baadaye yaani 75 imefungwa bao la nne kisha dakika ya 90 Marcus Rashford akapiga chuma ya tano.
Ushindi huo umezidi kuiweka England katika nafasi nzuri ya kufuzu Kombe la Dunia, lakini haijaihakikishia moja kwa moja.
Ufaransa imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Iceland licha ya kiungo wake Aurelien Tchouamen kuonyeshwa kadi nyekundu dakika 68, imejihakikisha walau nafasi ya kucheza mtoano kwa ajili ya kufuzu michuano hii.
Katika mechi nyingine za kufuzu Kombe la Dunia zilizopigwa ni pamoja na Cyprus dhidi ya Romania ambayo imemalizika kwa sare 2-2, Albania imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Latvia, Armenia ikaichapa Ireland mabao 2-1 wakati Bosnia ikiwa nyumbani ikakubali kufungwa mabao 2-1 mbele ya Austria.