Rashford kupunguza mshahara aondoke Man United
Mshambuliaji wa Man United ambaye anacheza Barcelona kwa mkopo, Marcus Rashford. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Akiwa Barcelona msimu huu, mshambuliaji huyu wa England ameonyesha kiwango bora akifunga mabao 13 na kutoa pasi 11 za mabao katika michuano yote.
Barcelona, Hispania. Mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford anadaiwa kuwa tayari kupunguza mshahara wake ili kuondoka kwa Mashetani Wekundu hao na kujiunga Barcelona.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania, nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 hana mpango wa kurejea tena United licha ya kuwa na mkataba unaoendelea hadi mwaka 2028, huku akielekeza nguvu zake kubaki kwa Mabingwa hao wa Hispania.
Ripoti zinaeleza kuwa dili la uhamisho lililokuwa linaonekana kukamilika mapema sasa lipo hatarini kuvunjika, baada ya Barcelona kutaka kupunguza ada ya uhamisho inayokadiriwa kufikia Paundi 26 milioni (Sh89 bilioni), wakati United wakigoma kushusha bei hiyo.
Hatua ya Rashford kukubali kupunguza mshahara wake mkubwa wa Paundi 325,000 (Sh1.2 bilioni) kwa wiki inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kulazimisha uhamisho huo, hasa ikizingatiwa Barcelona walikuwa tayari kubeba mzigo wa mshahara wake kwa kiwango kikubwa.
Akiwa Barcelona msimu huu, Rashford ameonyesha kiwango bora akifunga mabao 13 na kutoa pasi 11 za mabao katika michuano yote.
Pamoja na changamoto za muda wa kucheza kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa wa washambuliaji, nyota huyo anaelezwa kujisikia kuthaminiwa na kuwa sehemu ya kikosi anachokiona kuwa bora duniani.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, ameonekana kufurahishwa na mchango wa Rashford, ingawa amekuwa makini kutozungumzia hatma yake ya muda mrefu.
“Nina furaha na Marcus, ameonyesha ubora wake na amefunga mabao muhimu. Kuhusu mustakabali wake, kwa sasa tunazingatia mechi zilizobaki,” amesema Flick hivi karibuni.
Wakati huo huo, kurejea kwa Rashford United kunaweza kuathiri mpango wa kupunguza mishahara uliowekwa na mmiliki mwenza Sir Jim Ratcliffe, jambo linaloifanya klabu hiyo kuwa tayari kusikiliza ofa kwa mchezaji huyo.
Katika timu ya taifa ya England chini ya Thomas Tuchel, Rashford ameendelea kuwa sehemu muhimu, na anatarajiwa kuwa kwenye kikosi kitakachoelekea katika fainali za Kombe la Dunia lijalo.
Inaelezwa kuwa mshambuliaji huyo anataka mustakabali wake ujulikane mapema kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, ili kuondoa sintofahamu juu ya maisha yake ya soka.