Torres kumpisha Rashford Barcelona
Muktasari:
- Barcelona wanatafuta njia ya kuongeza fedha, ambapo wanafikiria kumuuza mshambuliaji wao Ferran Torres katika dirisha lijalo la usajili. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na klabu hiyo mwaka 2022 akitokea Manchester City.
Barcelona, Hispania. Barcelona inapanga kufanya mabadiliko katika kikosi chake kwa kumuuza mshambuliaji Ferran Torres katika dirisha lijalo la usajili ili kupata fedha za kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford.
Rashford kwa sasa yupo Barcelona kwa mkopo na ameonyesha kiwango kizuri tangu ajiunge na klabu hiyo ya Hispania, hali iliyomuwezesha hata kupata nafasi tena katika kikosi cha timu ya taifa ya England kinachoongozwa na Thomas Tuchel.
Hata hivyo, jitihada za Barcelona kumbakiza Rashford zimegonga mwamba kutokana na msimamo mkali wa Manchester United, ambao wamesisitiza kuwa hawako tayari kumtoa kwa mkopo tena bali wanataka kumuuza moja kwa moja, wakimthaminisha kwa Pauni 26 milioni (Sh89 bilioni).
Kutokana na hali hiyo, Barcelona sasa wanatafuta njia ya kuongeza fedha, ambapo wanafikiria kumuuza mshambuliaji wao Ferran Torres katika dirisha lijalo la usajili.
Mshambuliaji wa Barcelona, Ferran Torres ambaye anaripotiwa kuuzwa katika dirisha lijalo la kiangazi. Picha na Mtandao
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na klabu hiyo mwaka 2022 akitokea Manchester City, lakini bado hajawa tegemeo kubwa kikosini.
Barcelona wana hofu ya kumpoteza Torres bure siku zijazo kwani mkataba wake unaelekea ukingoni mwaka 2027, hivyo wanataka kumuuza mapema ili kuepuka hasara.
Wakati huo huo, klabu hiyo pia inapanga kufanya maboresho zaidi katika safu ya ushambuliaji, huku ikitarajiwa kumuongezea mkataba mshambuliaji mkongwe Robert Lewandowski, pamoja na kutazama uwezekano wa kumsajili mshambuliaji mwingine wa muda mrefu.
Miongoni mwa majina yanayotajwa ni Julian Alvarez wa Atletico Madrid, ambaye anaonekana kuwa chaguo la baadaye katika nafasi ya ushambuliaji.
Kwa upande wa Rashford, ameonyesha mchango mkubwa tangu ajiunge na Barcelona, akifunga mabao 10 na kutoa pasi za mabao 13 katika mechi 39 alizocheza katika mashindano yote.
Mshambuliaji wa Man United anayekipiga kwa mkopo Barcelona, Marcus Rashford, anaripotiwa kuuzwa moja kwa moja Barcelona mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika. Picha na Mtandao
Hata hivyo, bado anakabiliwa na ushindani mkali katika kikosi hicho cha kocha Hansi Flick, ambapo anashindana na wachezaji kama Raphinha na chipukizi Lamine Yamal.
Kuongezeka kwa matumaini ya Rashford kubaki Barcelona kumekuja pia kufuatia kuchaguliwa tena kwa rais wa klabu hiyo Joan Laporta, ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa mipango ya kocha Flick.
Awali, Rashford mwenyewe alieleza kuwa anafurahia maisha Barcelona na angependa kubaki, akisisitiza kuwa klabu hiyo inampa mazingira bora ya kushindana na kushinda mataji.
Hata hivyo, mustakabali wake bado upo mikononi mwa Manchester United, ambao wanaonekana kushikilia msimamo wao wa kumuuza moja kwa moja, hali inayoweza kuifanya Barcelona kulazimika kufanya maamuzi magumu ya kifedha ili kufanikisha dili hilo.