Prof Jay aipa neno zito Simba

Muktasari:
Simba ipo nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 62 sawa na Yanga inayoongoza kwa tofauti ya mabao pia ikiwa na mechi matatu mkononi.
Mwanamuziki na Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule 'Professa Jay' ameitaka timu yake ya Simba kuweka nguvu zaidi katika fainali ya Kombe la Shirikisho kuliko Ligi Kuu Bara.
Simba ipo nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 62 sawa na Yanga inayoongoza kwa tofauti ya mabao pia ikiwa na mechi matatu mkononi.
Profesa Jay licha ya kuiombea timu yake hiyo ichukue ubingwa wa Ligi Kuu, lakini alisema Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa bila wasiwasi ni Kombe la Shirikisho watakapocheza fainali dhidi ya Mbao kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Mei 28.
Profesa Jay ambaye ni Mbunge wa Chadema kupitia jimbo la Mikumi, Morogoro alisema ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba utatagemeana na mechi za Yanga kama watashinda mechi zao 3 zilizobaki watajihakikishia ubingwa huo tofauti na Simba yenye mechi mbili itakuwa ni kazi bure hivyo ni vyema zaidi kujipanga kwa fainali ya FA.
ìFuraha yangu ni kuona Simba inachukua ubingwa wa Ligi Kuu bara na ubingwa wa Shirikisho kutokana na ubora wa kikosi cha timu yetu hivyo tutashinda mechi zilizobaki na kutwaa ubingwa japo imani yangu kubwa zaidi ipo kwenye Kombe la Shirikisho,î alisema Profesa Jay.
Akizungumzia fainali ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa msanii huyo alilipongeza Shirikisho la Soka nchini {TFF} kwa kuileta fainali hiyo sasa wakati vikao vya Bunge vinaendelea.
Mbali ya kuwashangaa waliohoji fainali hiyo kuchezwa Dodoma, Mbunge huyo aliwataka wapenda soka kutoka mikoa mbalimbali nchini kufika kwa wingi siku ya fainali ya kombe hilo Mei 28 hususani wale wa Simba ili kushuhudia timu yao ikibeba ubingwa.
ìNaipongeza TFF kwa uamuzi wao wa kuileta fainali ya Kombe la FA mjini Dodoma kwani itatupa fursa wabunge kuiona fainali hiyo Uwanja wa Jamhuri uwanja una sifa zote wadau wasiogope hilo na pia niwaombe mashabiki wa Simba kutoka mikoani waje tuishangilie ubingwa wa timu yetu,î alisema Prof Jay.