Petit alia na Mbappe Euro 2024

Muktasari:

  • Maneno ya gwiji wa zamani wa Ufaransa, Emmanuel Petit yameonyesha ni wazi kutokana na mtazamo wake  Kylian Mbappe hana uwezo wa kuvaa kitambaa cha unadha.

Paris, Ufaransa. Gwiji wa Ufaransa, Emmanuel Petit amehoji kiwango cha Kylian Mbappe anachokionyesha kwenye kikosi cha Les Bleus kwenye Euro 2024.

Mbappe alichaguliwa kuwa nahodha wa Ufaransa kwa ajili ya fainali hizo za kusaka ubingwa wa Ulaya, huku kikosi hicho cha kocha Didier Deschamps kikitajwa kuwa moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa huo.

Timu hiyo ilimaliza kwenye nafasi ya pili kwenye Kundi B baada ya kutoka sare na Poland, Jumatatu iliyopita na hivyo kuwafanya Austria kuongoza kundi hili. Jambo hilo linafanya Les Bleus kuwa na njia ngumu kuelekea fainali ya Euro 2024, huku Mbappe akikosa mechi dhidi ya Uholanzi kutokana na kuvunjika pua. kabla ya kufunga bao lake la kwanza kwenye michuano hiyo kwa mkwaju wa penalti dhidi ya Poland.

Hata hivyo, si wote wanaovutiwa na kiwango cha soka lake, ambapo gwiji wa Ufaransa na mchambuzi wa soka, Petit hakusita kumkosoa mchezaji huyo, akisema kwamba majigambo yake pia yanaweza kuleta shida kwenye vyumba vya kubadilishia.

"Kuna timu yenye Mbappe na kuna nyingine isiyokuwa na Mbappe. Kuwa nahodha kunahitaji kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza wengine na si kutaka kuonekana wewe tu," alisema Petit.

"Hakuna ubishi Kylian Mbappe ni mchezaji bora kwenye timu na wenzake wanamsapoti, lakini kiongozi anapaswa kulionyesha hilo uwanjani."

Kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora, Ufaransa itakipiga na Ubelgiji ya Kevin De Bruyne, Jumatatu Julai Mosi mwaka huu.

Na kuhusu suala la Mbappe kutamba na Ufaransa hilo halina mjadala, ambapo staa huyo alifunga mabao 12 katika mechi 14 alizocheza kwenye Kombe la Dunia. Ufaransa ina mastaa wengi, lakini inahitaji Mbappe awe kwenye kiwango bora kabisa kufanya vizuri ndani ya uwanja.