Manji afariki dunia nchini Marekani

Aliyekuwa mwenyekiti na mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji

Dar es Salaam. Mwenyekiti na mfadhili wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji amefariki duniani jana Jumamosi Juni 29, 2024, huku mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Rage akiukumbuka ucheshi na mazungumzo waliyofanya wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Manji (49), ambaye alifariki dunia jana, saa sita, akiwa Florida, Marekani, miezi miwili iliyopita alifanya mahojiano marefu na gazeti hili ambapo alizungumza mambo mengi kuhusiana na soka, hususan timu za Yanga na Simba.

Mtoto wa marehemu, Mehabub Manji amelithibitishia Mwananchi kuhusu kifo cha baba yake akisema baba yake alianza kuungua ghafla na kwenda hospitali sehemu ambayo umauti ulimkuta.

"Kwa sasa nipo njiani nakwenda hospitali, lakini ukweli ni kwamba baba amefariki hapa Florida, Marekani. Nafikiri taarifa nyingine nitakupa baada ya kufika," amesema Mehabub ambaye alikuwa akiongozana na baba yake mara kwa mara walipokuwa jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti huyo wa zamani ambaye alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne akiwa na Yanga na kipindi chote timu ilifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika, anakumbukwa na mashabiki wa timu hiyo kama mmoja kati ya viongozi wenye mafanikio makubwa zaidi Jangwani.

Manji ambaye aliingia madarakani siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba, Mei 6, 2012 alifanya kazi kubwa kipindi cha uongozi ikiwamo kuhakikisha anavunja makundi mawili makubwa yaliyokuwa yanapingana ndani ya timu hiyo moja likiitwa Yanga Asili na lingine Yanga Kampuni.

Manji aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017, anakumbukwa na wana Yanga kwa kufanikiwa kuwasajili wachezaji wakubwa kama Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emannuel Okwi, Thaabani Kamusoko, Obrey Chirwa na Donald Ngoma kwenye kikosi chake.

Mbali na wachezaji mahiri ambao walisajiliwa, Manji pia aliajiri makocha kadhaa wakubwa wakiwemo Konstadian Papic, Milutin Sredojevic Micho, Sam Timbe, Ernest Brandts na Tom Santifiet na kuleta mabadiliko makubwa katika soka la Tanzania.

Mfanyabiashara huyo ambaye alijiuzulu uenyekiti Yanga, Mei 21, 2017 katika mahojiano yake ya hivi karibuni na gazeti hili alisema anaamini Simba kwa sasa inashindwa kufanya vizuri baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Pope ambaye aliamini alikuwa na ubora wa hali ya juu kutambua wachezaji mahiri sokoni.


Rage, Chambua wamlilia

Akizungumzia kifo cha Manji, nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amesema mfanyabiashara huyo atabaki katika mioyo ya wapenzi wa timu hiyo kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya baada ya kupitia kipindi kigumu.

"Ni taarifa ya huzuni sana kwa wanamichezo kwa sababu Manji aliandika historia ya kuifanya Yanga kuwa timu tishio, kwa sababu kama unakumbuka kabla ya kuingia kwake madarakani timu ilipitia changamoto kubwa ya kuandamwa na ukata wa kifedha na kuja kubadilisha hali ya uchumi wa klabu," amesema Chambua.

Ameongeza kuwa atamkumbuka Manji kwa mengi ikiwamo nia yake ya kutaka kumfundisha ukocha nchini England kipindi akiwa Yanga ndoto ambayo haijatimia.

"Yanga nimeitumikia kwa miaka 14, 10 nikiwa kama mchezaji na minne nikiwa kama kocha. Nakumbuka alitaka kunipeleka nchi ya England kwa ajili ya masomo zaidi ya ukocha, japo sikufanikiwa hilo ila namkumbuka kwa moyo wake mzuri juu yangu."

Kwa upande wake, Rage ambaye alikuwa mwenyekiti wa Simba wakati wa utawala wa Manji alisema licha ya kusikitiswa na kifo cha Manji, lakini anakumbuka upinzani wa timu walizoziongoza au kuzishabikia na pia walikuwa marafiki walioheshimiana.

"Alikuwa mtu mcheshi na asiyekuwa na makuu. Nakumbuka wakati wa uongozi wetu nililazwa Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam kwa bahati nzuri na yeye alikuwepo hivyo tukawa chumba kimoja, tukawa tunazungumza kama ndugu. Kiukweli nimeumia baada ya kusikia taarifa hiyo."