Huyu ndiye Yusuf Manji wa 1975 mpaka 2024

Mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Manji alifariki dunia jana Juni 29, 2024 Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa akipatiwa matibabu akiwa na umri wa miaka 49.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji amefariki dunia Jumamosi Juni 29, 2024 saa 6 usiku katika Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa anapatiwa matibabu.

Manji (49), ambaye alifariki dunia saa sita usiku akiwa miezi miwili iliyopita alifanya mahojiano marefu na Mwananchi Digital ambapo alizungumza mambo mengi kuhusiana na soka, hususani timu za Yanga na Simba.

Mtoto wa marehemu, Mehabub Manji alilithibitishia Mwananchi kuhusu kifo cha baba yake akisema alianza kuugua ghafla na kwenda hospitali sehemu ambayo umauti ulimkuta.

"Ukweli ni kwamba baba amefariki hapa Florida, Marekani. Nafikiri taarifa nyingine nitakupa baadaye," alisema Mehabub ambaye alikuwa akiongozana na baba yake mara kwa mara walipokuwa jijini Dar es Salaam na kwenye mechi za Yanga kwa Mkapa.

Mwenyekiti huyo wa zamani ambaye alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne 2012/2013 na mara tatu mfululizo 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017.

Pia, alifanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho FA na Kombe la Kagame 2012 likiwa ndiyo kombe la mwisho la michuano hiyo kwa Yanga.

Akiwa na Yanga kipindi chote timu ilifuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ingawa haikufanya vizuri sana, anakumbukwa na mashabiki wa timu hiyo kama mmoja kati ya viongozi wenye mafanikio makubwa zaidi Jangwani lakini akiwa mmoja kati ya watu walioleta mapinduzi ya soka Tanzania.

Manji ambaye aliingia madarakani siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Mei 6, 2012 alifanya kazi kubwa kipindi cha uongozi ikiwamo kuhakikisha anavunja makundi mawili makubwa yaliyokuwa yanapingana ndani ya timu hiyo moja likiitwa Yanga Asili na lingine Yanga Kampuni.

Manji aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017 baada ya kukwaruzana na wazee wa timu hiyo akiwemo marehemu Yahaya Akilimali, anakumbukwa na wana Yanga kwa kufanikiwa kuwasajili wachezaji wakubwa kama Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emannuel Okwi, Thaabani Kamusoko, Obrey Chirwa na Donald Ngoma kwenye kikosi chake.

Mbali na wachezaji mahiri ambao walisajiliwa, Manji pia aliajiri makocha kadhaa wakubwa wakiwemo Konstadian Papic, Milutin Sredojevic Micho, Sam Timbe, Ernest Brandts, Marcio Maximo, George Lwandamina na Tom Santifiet na kuleta mabadiliko makubwa katika soka la Tanzania.

Mfanyabiashara huyo ambaye alijiuzulu uenyekiti Yanga, Mei 21, 2017 katika mahojiano yake ya hivi karibuni na gazeti hili alisema anaamini Simba kwa sasa inashindwa kufanya vizuri baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Pope ambaye aliamini alikuwa na ubora wa hali ya juu kutambua wachezaji mahiri sokoni.

“Simba ni timu kubwa Tanzania, ina fanbase kubwa sana lakini mimi naamini kuwa inashuka kwa sasa kwa kuwa mtu mmoja muhimu sana hayupo. Ukitazama utagundua kuwa Simba imeanza kushuka tangu alipofariki Zacharia Hans Pope, huyu alikuwa mtu wa tofauti sana lakini alikuwa anajua ni mchezaji gani anatakiwa kwa kipindi gani.

“Pamoja na kwamba alikuwa na timu yake na mimi yangu, lakini tulikuwa marafiki wakubwa na mara kwa mara tulikuwa tukikutana tunazungumza kama ndugu bila kuweka Usimba na Uyanga wetu,” ilikuwa kauli ya mwisho ya Manji alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi Dijital.

Hata hivyo, katika mahojiano hayo Manji alisema alifanikiwa kutazama  michezo miwili ya Yanga ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns na mchezaji wake mahiri kuliko wote aliyemuona kwenye kikosi cha Yanga ni Stephen Aziz Ki.

 “Nilifanikiwa kuutazama mchezo ule wa Yanga kule Afrika Kusini dhidi ya Mamelodi ambao Yanga ilifungwa kwa penalti, niliwaona wamecheza vizuri sana, lakini kuna mchezaji mmoja nilimuona ana nywele za Blonde (blichi), alionyesha kiwango cha juu sana na nimemuona pia kwenye mechi ya Dabi.

“Sijamfahamu vizuri jina lake, unajua siku hizi siyo kama zamani, sasa navaa miwani na umri umeenda,” Alipoonyeshwa picha tofauti za wachezaji wa Yanga alipomuona Aziz Ki alisema:“ Huyohuyo ndiye ninamaanisha huku akicheka, anakwenda uwanjani akijua nini anakwenda kufanya, ndiye ananivutia sana akiwa na Yanga nafikiri kila mmoja atakubaliana nami.”

Mara baada ya Manji kujiuzulu klabu hiyo ilipita kwenye ukata mkubwa ambapo ilianza kutembeza bakuli kwa ajili ya kujiendesha ambapo lilipewa jina la Kubwa Kuliko na kuhamishia utawala wa soka la Tanzania kwa Simba ambayo ilitwaa ubingwa wa ligi mara nne mfululizo na Azam mara moja, hadi timu hiyo ilipopata uwekezaji wa GSM ndiyo ikarejea kwenye makali yake ya kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo hadi msimu uliopita.


Wasifu wa Hayati Yusuf Manji

Alizaliwa Oktoba 14, 1975 katika Jiji la Dar es Salaam, Tanzania

Mwaka 1995 alianzisha kampuni ya Quality Group Limited iliyofahamika Tanzania na Afrika kwa kusambaza bidhaa mbalimbali.

Alisoma shahada ya uhasibu kutoka Chuo cha Hofstra kilichopo jiji la New York, Marekani.

Mwaka 2015, alichaguliwa kuwa Diwani wa Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)

Enzi za uhai wake, Manji alifanikiwa kupata watoto wawili

Aliiongoza Yanga kwa miaka mitano akiingia madarakani 2012 na kujiuzulu 2017

Anakumbukwa na Wana Yanga kwa kutwaa mataji manne ya ligi kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la Kagame na kuwasajili wachezaji wakubwa kama Kelvin Yondani, Juma Kaseja na Emannuel Okwi na wengine wengi.

Amefariki dunia Juni 29, 2024 Jimbo la Florida nchini Marekani alipokuwa akipatiwa matibabu.

Manji amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49.