Mbappe hatarini kuzikosa mechi zote za makundi Euro

Muktasari:

  • Mbappe ambaye alivunjika pua katika mchezo wa hatua ya makundi wa michuano ya Euro dhidi ya Austria baada ya kugongana na beki Kevin Danso dakika ya 90, alishindwa kuendelea na mchezo huo, akatolewa nje kuwahishwa Hospitalini.

DUSSELDORF, UJERUMANI. Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, staa wa Ufaransa na Real Madrid, Kylian Mbappe anaweza kutocheza mechi zote za michuano ya Euro 2024, zilizosalia baada ya kufanyiwa upasuaji wa pua utakaomweka nje kwa zaidi ya siku 10.

Mbappe ambaye alivunjika pua katika mchezo wa hatua ya makundi wa michuano ya Euro dhidi ya Austria baada ya kugongana na beki Kevin Danso dakika ya 90, alishindwa kuendelea na mchezo huo, akatolewa nje kuwahishwa Hospitalini.

Daktari wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa Fabrice Bryand aliliambia gazeti la L’Equipe kwamba staa huyo anaweza kukaa nje kwa siku 10 hali ambayo itamfanya kukosa mechi zote za hatua ya makundi na kama Ufaransa haitofuzu kwenda hatua inayofuata, basi huo ndio utakuwa mwisho wake katika  michuano ya mwaka huu.

Muda mchache baada ya kusambaa picha zilizomuonyesha anatoka nje ya uwanja huku akuvuja damu puani, Shirikisho la mpira wa miguu la Ufaransa, lilithibitisha kwamba ni kweli Mbappe alivunjika pua na amefanyiwa upasuaji.

Hakuna taarifa kamili juu ya wapi upasuaji huo ulifanyika lakini taarifa zinadai zinadai kuwa ni katika hospitali ya University Hospital of Düsseldorf.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alipoulizwa juu ya hali ya staa huyu alisema:"Bado haendelei vizuri, inabidi tusubiri tuon4e itakuwaje, siwezi kutoa jibu linalo eleweka kwa sasa, bado yupo chini ya uangalizi wa timu ya madaktari, pua yake imevunjika vibaya"

Katika mchezo huu Ufaransa iliibuka na ushindi wa bao 1-0, ambalo lilikuwa ni la kujifunga kwa beki Maximilian Wober dakika ya 38.

Mbali ya mechi hii, jana pia kulikuwa na mechi nyingine za Euro ambapo Romania ilicheza na Ukraine na kuichapa mabao 3-0, kisha Ubelgiji ikapoteza mbele ya Slovakia kwa bao 1-0.