Deschamps aingiwa ubaridi jeraha la Mbappe

Muktasari:

  • Mbappe alirejea uwanjani jana na kuifungia timu yake bao ambalo liliipelekea Ufaransa kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Poland.

Lepizig, Ujerumani. Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps amefunguka na kuibainisha wasiwasi wake juu ya mchezaji Kylian Mbappe kucheza akiwa amevaa maski, hilo linaloweza kumfanya asiwe na uono mzuri kwenye fainali za Euro 2024.

Mbappe alivunjika pua kwenye mechi ya kwanza ya Ufaransa ilipokipiga na Austria, lakini siku za karibuni alionekana kufanya mazoezi akiwa amevaa maski na ilitazamwa kama usiku wa jana Jumanne, angecheza kwenye mchezo dhidi ya Poland.

Alikosa mechi ya Uholanzi, hivyo mashabiki walimsubiri kwa mchezo wa jana dhidi ya Poland uliochezwa huko Dortmund na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ambapo yeye ndiye alifunga bao hilo kwa penalti kabla ya wapinzani nao kuchomoa kwa penalti.

Alipoulizwa kama maski itakuwa na msaada kwa supastaa huyo, Deschamps alisema: “Kupumua sio shida, lakini kuona nadhani itakuwa shida. Sijawahi kucheza na maski, lakini navuta hisia kwa wale wanaovaa, nahisi kama hawapo na uhuru sana.

“Nachokiona ni kama kinazuia kidogo uono wako. Ni wazi kunakuwa na vikwazo kwenye uono.”

Kocha Deschamps aliulizwa alishindwa kuweka mambo hadharani kuhusu mshambuliaji huyo kama angetumika kwenye mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya Poland, ambayo tayari imeshaaga fainali hizo za Euro 2024.

"Anaendelea vizuri siku hadi siku," alisema Deschamps.
"Juzi tulikuwa wote mazoezini na majeraha yake kwenye pua yalionekana kukauka. Itamlazimu kuzoea kucheza na maski.

Yeye anataka kucheza kila mechi, alitaka kucheza ile ya Uholanzi na alitaka pia kucheza dhidi ya Poland."

Ufaransa imemaliza hatua ya makundi ikiwa imefunga mabao mawili kwenye Euro 2024 ambapo moja ni la mchezaji wa Austria, Maximilian Wober kujifunga huku lingine likifungwa na Mbappe kwa penalti huku pia timu hiyo ikiruhusu bao moja.