Mbappe anasubiri jambo moja PSG

Muktasari:
- Ubingwa wa kombe hilo msimu huu, ndio pekee unaoweza kumfutia Mbappe aibu ya kuwa miongoni mwa nyota watatu ambao wamekuwa watumishi hewa klabuni hapo
Paris,Ufaransa. Taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya linaweza kuwa pekee la kumfanya Kylian Mbappe ajitofautishe na Lionel Messi, Neymar waliofeli kutimiza lengo la mabilioni ya fedha la PSG ambalo ni kutwaa taji hilo.
Ubingwa wa kombe hilo msimu huu, ndio pekee unaoweza kumfutia Mbappe aibu ya kuwa miongoni mwa nyota watatu ambao wamekuwa watumishi hewa klabuni hapo katika kipindi cha miaka saba kwa kushindwa kuipatia PSG taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kitendo cha nyota huyo kutangaza kuwa ataachana na PSG baada ya msimu huu kumalizika kinamlazimisha kuhakikisha anaiongoza kutwaa taji la mashindano hayo ambalo hapana shaka limekuwa likitamaniwa na mataikuni wa timu hiyo kutoka Saudi Arabia ambao walifanya uwekezaji mkubwa wa fedha katika kipindi cha miaka saba wakiamini watafanikiwa kulichukua.
Baada ya tetesi za muda mrefu, Mbappe alibainisha wazi kuwa hatosaini mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo, jambo linaloashiria kuelekea kuanguka kwa mpango ambao wamiliki wa timu hiyo waliuandaa hapo awali na hivyo kufungua milango ya mkakati mpya.
Ndani ya muda wa miaka saba, PSG iliwekeza kiasi cha Pauni 807 milioni kwa Neymar, Mbappe na Lionel Messi ambao ilionekana kama wangekuwa msaada mkubwa kwa miamba hiyo ya Ufaransa katika vita ya kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kana kwamba haitoshi, timu hiyo ilitumia kiasi cha Pauni 537 milioni kwa ajili ya usajili na mishahara ya nyota wengine wa kuwaongezea nguvu watatu hao.
Lakini hata hivyo, mambo yameonekana kwenda tofauti kutokana na PSG kushindwa kutimiza lengo la kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya na bila shaka kuondoka kwa Mbappe kutakuwa pigo kubwa kwa klabu hiyo na litatafsiri kwamba amekuwa anguko la mkakati wake wa miaka saba.
Tofauti na wenzake Messi na Neymar, Mbappe anayo nafasi ya kujitofautisha nao kwani PSG bado wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo kwa sasa timu hiyo ipo katika hatua ya 16 bora ikipangwa kukutana na Real Sociedad ambapo imeshashinda mchezo wa kwanza.
Ila kama PSG itashindwa kunyakua taji hilo, hakuna namna ambayo Mbappe ataweza kukwepa lawama za kuwa miongoni mwa walioiangusha PSG licha ya mchango mkubwa alioutoa katika mashindano tofauti ya ndani.
Haondoki patupu
Mbali na historia mbaya ya kushindwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa, Mbappe amefanikiwa kuiongoza PSG kutwaa idadi kubwa ya mataji ya ndani kulinganisha na Neymar na Messi ambao hawakutoa kitu kikubwa ndani ya timu kuendana na ubora na uzoefu wao.
Na hilo linaweza kuthibitishwa na tuzo nyingi binafsi ambazo Mbappe ameapata ndani ya PSG kulingana na nyota hao wawili ambao alikuwa akiunda nao utatu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Ameshinda mataji matano ya Ligi Kuu ya Ufaransa, mataji matatu ya Coupe de France, tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ufaransa mara nne, tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ufaransa mara tano, kuingia katika kikosi bora cha Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu pamoja na mchezaji bora wa Ufaransa mara tatu.
Lakini pia nyota huyo amefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa Ligi Kuu ya Ufaransa mara tatu huku akichukua tuzo ya mfungaji bora wa Ulaya mara moja.
Upande wa maslahi binafsi, Mbappe haondoki kinyonge kwani akaunti zake zinaonekana kunona kutokana na kile anachokichuma ndani ya timu hiyo.
Mchezaji huyo analipwa kiasi cha Pauni 888000 kwa wiki huku akiwa na utajiri unaoakadiriwa kufikia Pauni 180 milioni.
Uelekeo mpya
Ripoti zinafichua kuwa nyota huyo yuko mbioni kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho huru na alishafikia makubaliano zamani ya kujiunga na miamba hiyo.
Hilo linaweza kuthibitishwa na kauli za Rais wa Bodi ya Ligi Kuu Hispania 'La Liga' Javier Tebas pia Rais wa Real Madrid, Fiorentino Perez kuwa klabu hiyo iko imara kiuchumi kuweza kumsajili Mbape.
"Itategemea na Real Madrid, mwenyekiti na kile anachotaka kukibashiri. Kama mchezaji anataka kujiunga nao, ni asilimia 50 inawezekana," alisema Tebas.
Nuksi ya mastaa
Ikiwa atashindwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na PSG na kisha akaendelea kulikosa huko kwingine, atafuata nyayo za mastaa wa soka ambao walikuwa hawana bahati ya kulishika taji la mashindano hayo.
Mfano wa mastaa wa soka ambao wamepishana na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Ronaldo De Lima, Zlatan Ibrahimovic, Gabriel Batistuta, Hernan Crespo, Cesc Fabregas, Michael Ballack, Michael Ballack, Pavel Nedved, Lilian Thuram, Francesco Totti, Fabio Cannavaro, Eric Cantona, Patrick Vieira, Gianluigi Buffon na Dennis Bergkamp.