Ntibazonkiza aendelea kukomaa akikabidhiwa mikoba Burundi
Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Saido Ntibazonkiza akiwa amevalia jezi ya timu ya Taifa ya Burundi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Burundi itacheza na Chad, ugenini, Machi 26, 2026 na timu hizo zitarudiana jijini Bujumbura, Machi 31, 2026.
Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Saido Ntibazonkiza ameendelea kuwa lulu kwa timu ya taifa ya Burundi baada ya kujumuishwa katika kikosi chake kinachojiandaa na mechi mbili za hatua ya awali ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Chad baadaye mwezi huu.
Kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 38, ameshaitumikia timu ya taifa ya Burundi kwa miaka 22 tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Burundi, Patrick Mayani, ameamua kumjumuisha Ntibazonkiza anayeichezea Vital’O ya Burundi ambaye tangu Novemba 2024, alikuwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo.
Kikosi hicho kinajumuisha nyota wawili wanaocheza Ligi Kuu ya NBC ambao ni kiungo Elie Mokono wa Fountain Gate na Nduwumwe Mossi wa Singida Black Stars.
Kipa wa zamani wa Namungo FC ambaye kwa sasa anaitumikia Vision FC ya Burundi, Jonathan Nahimana ni miongoni mwa wachezaji ambao wameitwa katika kikosi cha Burundi ambacho kinajumuisha nyota 26.
Burundi itacheza na Chad, ugenini, Machi 26, 2026 na timu hizo zitarudiana jijini Bujumbura, Machi 31, 2026.
Kikosi cha Burundi kinaundwa na makipa Jonathan Nahimana, Onesime Rukundo na Daniel Hakizimana huku mabeki wakiwa ni Kevin Icoyitungiye, Moussa Omar, Djuma Nzeyimana, Claus Niyukuri, Nsabiyumva Frederic, Christophe Nduwarugira, Muderi Akbar na Youssuf Ndayishimiye.
Viungo ni Mukono, Abdulkarim Mpawenimana, Msanga Henry, Bizoza Parfait, Ntibazonkiza na Abedi Bigirimana.
Washambuliaji ni Bienvenue Kanakimana, Jean Claude Girumugisha, Franck Nduwimana, Ndikumana Asman, Liongola Jordi, Ineza Abdi, Amissi Cedric na Nduwumwe Mossi.