Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namba 13 ilivyogeuka tatu kwa Sowah



Inaweza ikawa ngumu kuamini lakini mambo ndivyo yalivyo hadi sasa kwa mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah ambaye alitua Klabuni hapo kwa mbwembwe nyingi akitokea kwa walima Alizeti, Singida Black Stars ambapo alitumika kwa nusu msimu pekee akionesha kiwango kikubwa na kuwavutia vigogo hao wa Kariakoo kumnunua katika dirisha la kiangazi lililopita.

Sowah alivyotua Msimbazi alionekana kwenda kukata kiu ya wanasimba ya kuwa na Straika kiongozi katika kikosi chao tangu walipoondoka Mnyarwanda, Medie Kagere, nyota wa DR Congo, Chris Mugalu na mwingine ni Mtanzania, John Bocco ambao walionesha makali ya kufumania nyavu katika nafasi hiyo, lakini tangu walipoondoka washambuliaji hao kumekuwa na pengo katika nafasi hiyo ambayo wamekuja washambuliaji tofauti lakini wameshindwa kuitendea haki kama walivyofanya nyota wengine.

Ujio wa Sowah ndani ya Simba ulionekana kwenda kutibu tatizo hilo kutokana na namba 13 alizokujanazo kutokea Singida Black Stars, wengi walijiuliza kwamba, kama mshambuliaji huyo alicheza kwa nusu msimu Singida Black Stars na kuonesha kiwango cha hali ya juu namna ile je, kama ametua Msimbazi katika timu kubwa yenye wachezaji wakubwa na wenye uzoefu, kiwango chake kitaongezeka zaidi?

Na ndivyo ambavyo ni ngumu kuamini hadi sasa kwanini mshambuliaji huyu anashindwa kupata namba ndani ya kikosi cha Simba akisugua benchi licha ya kutua Klabuni hapo kwa kishindo kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya Singida Black Stars.


ALICHOKIFANYA SINGIDA BLACK STARS

Alipotua Singida Black Stars katika dirisha dogo la msimu uliopita ambapo alijiunga na timu hiyo akiktokea katika Klabu ya Medeama ya kwao Ghana, Sowah alionesha kiwango cha hali ya juu akitumia michezo 14 kufunga jumla ya mabao 13 katika Ligi Kuu Bara akicheza jumla ya dakika 477. Nyota huyu alifanikiwa kumaliza ligi akiwa nafasi ya tatu katika chati ya wafungaji bora akilingana na Leonel Ateba na Steven Mukwala wa Simba pamoja na Prince Dube wa Yanga ambao walimaliza na idadi sawa ya mabao huku wakiwa wamecheza mechi nyingi kuliko Sowah.

Kasi hiyo ya upachikaji mabao bila shaka ndio iliyowafanya Simba kuinasa saini ya mshambuliaji huyo na kuwaruhusu Ateba na Mukwala kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine wakiwa na matumaini zaidi na Sowah ambaye mpaka sasa anaonekana kuwa mzigo ndani ya Klabu hiyo huku kukiwa na tetesi kwamba huenda katika dirisha lijalo la usajili Simba wakamwachia mchezaji huyo huku juhudi za kumsaka mshambuliaji mwingine zikiwa zimeshaanza.


KINACHOENDELEA MSIMBAZI

Akiwa Simba, msimu huu timu hiyo ikiwa imeshacheza mechi 30 za mashindano tofauti msimu huu (Ligi ya Mabingwa 10, Ligi Kuu Bara 14, Kombe la Mapinduzi 3, Ngao ya Jamii 1 na Kombe la Shirikisho la CRDB mechi 2), Sowah amecheza mechi 11 kwa dakika 477.

Mechi hizo ni Ligi Kuu Bara (4), Ligi ya Mabingwa Afrika (6) na Kombe la Mapinduzi (1) ambapo mshambuliaji huyo amefanikiwa kufunga mabao matatu yote kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, JKT Tanzania na Mbeya City.

Simba iliamini kama Sowah alifunga mabao hayo akiwa Singida tena nusu msimu, basi anaweza kufunga zaidi akiwa kwao lakini matarajio hayo yamekuwa tofauti na kile ambacho kinaonekana sasa akiwa ndani ya jezi ya Wekundu wa Msimbazi.

Hata hivyo, ukiangalia vizuri takwimu hizo utagundua kuwa nyota huyu wa Kimataifa wa Ghana ameonesha kushuka kiwango kwani katika mechi 11 alizocheza hadi sasa na namba za mabao aliyoyafunga haviendani na kiwango alichokionesha katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita ambapo amebakiza mechi tatu kufikia idadi ya mechi 14 alizocheza msimu uliopita akiwa na Singida Black Stars katika Ligi Kuu.

Ukiacha hilo, kiufundi Sowah ameshindwa kutoboa ndani ya kikosi cha kwanza cha Simba chini ya makocha watano msimu huu kuanzia Fadlu Davids, Dimitar Pantev, Hemed Suleiman, Seleman Matola na sasa Steve Barker.

Makocha wote wamekuwa wanaonyesha kutokukubaliana na kiwango cha Sowah ambapo hata alipoanzishwa alitolewa mapema bila ya mshambuliaji huyo kuonyesha kitu kikubwa sana uwanjani.


MATUKIO YA UTATA

Sowah ndani ya muda ambao amekaa Simba amekumbana na matukio mawili ya kusimamishwa, akianza kukosa mechi za kwanza za ufunguzi wa ligi baada ya kupewa kadi nyekundu msimu uliopita kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB akiwa Singida akicheza dhidi ya Yanga.

Adhabu hiyo ilianza kuja kutumika akiwa Simba ambapo ilimfanya mshambuliaji huyo kukosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na wekundu hao wakapoteza kwa bao 1-0, huku wakikosa huduma ya mshambuliaji ambaye waliamini angewasaidia.

Baada ya hapo akaja kusimamishwa na Kamati ya Usimamizi wa Ligi kwa mechi tano baada ya kumpiga kiungo wa Azam, Himid Mao, akakaa tena nje huku klabu yake ikiendelea kukosa huduma yake kwa mechi nne za ligi na moja Kombe la FA.

Kadi hizo ndani ya Simba zimechukuliwa kwa tofauti baada ya mabosi wa Wekundu kuona kama mshambuliaji huyo anazipata kirahisi hasa kutokana na kwamba yapo matukio ambayo hakupata adhabu kama hiyo lakini alionyesha kukaribia kukumbana na maamuzi ya namna hiyo.

Sowah pia alihusishwa kuchelewa kwenye mikutano kadhaa ya timu, kukataa kufanya mazoezi ya ziada, kuchelewa mazoezini, kusafiri kwenda Angola kucheza dhidi ya Petro Atletico akiwa amevaa jezi ya SL Benfica badala ya mavazi rasmi ya klabu. Mwisho ni kufanya faulo za makusudi zinazoweza kusababisha kadi nyekundu, ikiwemo kwenye mechi dhidi ya Azam FC na Espérance.


KINACHOMSUBIRI

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kinaeleza kuwa kwa sasa Klabu hiyo haioni kabisa mwanga wa kupata kile ilichokitarajia kutoka kwa Sowah na wanaona ni mchezaji ambaye anapasua gurudumu la timu wakati safari inaendelea, hatua ambayo hivi karibuni ilimfanya kusimamishwa kuendelea kuitumikia Klabu hiyo huku taarifa nyingine zikieleza kuwa Simba ipo mbioni kumtafuta Straika mwingine atakayekuja kuziba pengo lake msimu ujao.